Mbunge wa
Jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo Mhe. Dkt. Florence Samizi amesema filamu
maarufu ya Tanzania The Royal Tour iliyochezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta matokeo makubwa Katika Pori
la Akiba Moyowosi linalosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini
- TAWA wilayani humo kutokana na ongezeko kubwa la wageni wa uwindaji wa
kitalii wanaotembelea hifadhi hiyo na kuiingizia Serikali mapato makubwa.
Dkt.
Florence ameyasema hayo Septemba 27, 2024 wakati wa ziara ya mafunzo kwa ajili
ya madiwani wa Halmashauri ya Kibondo, Kamati ya siasa ya Kibondo (W) na
Sekretarieti ya Kibondo (W) ikiwa na
lengo la kuwawezesha kuona jitihada zinazofanywa na Serikali katika kusimamia
rasilimali za wanyamapori pamoja na
uendelezaji wa shughuli za uhifadhi hifadhini humo Kwa kuzingatia ilani ya CCM.
Ziara iliyoratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na kusimamiwa na TAWA.
Mbunge huyo
amesema kutokana na jitihada za Mhe. Rais Samia kutangaza utalii wa nchi yetu
na kuupa kipaumbele hifadhi ya Moyowosi imetia fora mwaka huu Kwa kupata idadi
kubwa ya wageni wa uwindaji wa kitalii na ongezeko kubwa la mapato.
"Hii
Hifadhi ya Moyowosi imekuwepo miaka mingi lakini ilikuwa haijafanya vizuri Kwa
kutia fora kama ilivyofanya mwaka huu (2024)," amesema Dkt. Florence.
"Tumepata
taarifa kwamba Mwaka 2022/23 walipata wageni 39 tu lakini mwaka huu wamepata
wageni 89 mara 3 ya wageni waliopata mwaka uliopita lakini pia mapato
yameongezeka ambapo mwaka 2022/23 hifadhi ilipata mapato ya bilioni 2.4 kwa
mwaka. Lakini leo tunapoongea hata mwaka haujaisha tayari hifadhi imeshakusanya
bilioni 3 kutokana na shughuli za uwindaji wa kitalii," ameongeza.
Samizi
amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Kwa Kazi kubwa aliyoifanya ambayo
imepelekea ongezeko kubwa la watalii nchini na kusisitiza si watalii wa utalii
wa picha pekee bali hata watalii wa uwindaji wa kitalii nao wameongezeka na
kupelekea jamii zinazozunguka hifadhi ya Moyowosi kunufaika kwa mapato hayo.
Akizungumzia
namna jamii inayozunguka hifadhi hiyo inavyofaika na shughuli za utalii, Mhe.
Dkt. Florence amesema Kwa kipindi cha mwaka 2024 vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo tayari
vimeshapokea shilingi Milioni 89 ambazo zimetumika Katika kuibua miradi
mbalimbali ikiwemo miradi ya ujenzi wa madarasa, ujenzi wa ofisi za Serikali za
vijiji, madawati pamoja na ununuzi wa
viti vya watu wenye ulemavu.
Awali akitoa
maelezo kuhusu Hifadhi ya Moyowosi Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Kanda ya
Magharibi Wilbright Munuo amesemea Hifadhi ya Moyowosi imekuwa na faida kubwa
kwa vijiji jirani vinavyoizunguka kutokana na mapato makubwa inayoiingizia
Serikali ambayo Kwa asilimia kubwa yanarudi kwa jamii.
"Sote
tumeona kwamba Hifadhi hii ina faida kubwa, kwa mwaka tu wa fedha uliopita
imekusanya zaidi ya bilioni 3, lakini pia zaidi ya milioni 134 zimeenda pia
kwenye Halmashauri ya Kibondo ikiwemo zaidi ya millioni 89 ambazo zimetokana na
ada ya wanyamapori lakini zaidi ya millioni 45 ambazo zimetokana na dola 5,000
ambazo zinalipwa kutoka Katika kila kitalu cha uwindaji kinawindisha Katika
Pori la Akiba Moyowosi.”
Munuo
ameongeza kusema kuwa Katika jitihada za kuongeza mapato ya Hifadhi hiyo, Moyowosi
imekuwa miongoni mwa hifadhi zilizoingizwa Katika mpango wa biashara ya hewa
ukaa.
Aidha,
ametoa wito Kwa washiriki wa ziara hiyo kupeleka ujumbe kwa jamii kuacha
vitendo vya uhalifu Katika hifadhi hiyo ikiwemo kuchungia mifugo, uharibifu wa
mimea, ujangili wa wanyamapori pamoja na uvuvi haramu huku wakiwasisitiza
kuunga mkono jitihada za Serikali katika shughuli za uhifadhi na uendelezaji wa
shughuli za utalii sambamba na kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Na. Beatus Maganja- TAWA
0 Maoni