WAZIRI MKUU
Kasimu Majaliwa amehutubia Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
(UNGA79) na kusema Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ni msingi wa matumaini
katika kukabiliana na changamoto za kidunia.
Hii ni mara
ya pili kwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
ambapo mara ya kwanza ilikuwa Septemba 27, 2010 wakati Waziri Mkuu Mstaafu,
Mizengo Kayanza Pinda alipolihutubia Baraza la 65 (UNGA65).
Ametoa kauli
hiyo jana (Ijumaa, Septemba 27, 2024) wakati akihutubia kwenye Mkutano Mkuu wa
Mwaka huu wa Umoja wa Mataifa wa Wakuu wa Nchi mbalimbali za dunia jijini New
York, Marekani anakomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alisema chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, Tanzania imedhamiria kufanikisha malengo endelevu ya kiuchumi, ufugaji, uwekezaji katika miundombinu na mifumo ya kidijitali, uvuvi na nishati.
“Lengo letu
ni kufikia uhakika wa kupunguza umasikini, kutengeneza ajira mpya na kusukuma
mbele maendeleo ya uchumi shirikishi katika nyanja mbalimbali,” alisema na
kuongeza kwamba kuna shuhuda nyingi za taarifa za makuzi katika sekta hizo
nchini Tanzania zinazotokana na mikakati kama ya Kesho Iliyo Bora (BBT)
unaohusu kilimo kwa Tanzania Bara na uwezeshaji wanawake wanaoshiriki kilimo
cha mwani Zanzibar.
Alisema
Tanzania, kama yalivyo mataifa mengine, imekuwa ikipambana na changamoto kama
za athari za ugonjwa wa uviko (COVID 19), kwenye sekta ya afya, mabadiliko ya
tabianchi yanayojidhihirisha katika ongezeko la hali mbaya ya hewa kama mvua
haribifu na ukame uliokithiri, pamoja na mambo mengine, vimeathiri ufikiwaji wa
malengo endelevu.
Waziri Mkuu
Majaliwa alizungumzia pia Sera ya Tanzania ya Mambo ya Nje kuhusu utu, kwamba
Desemba 14, 1961, wakati akiwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, Mwalimu Julius
Nyerere alisema: “Msingi wa matendo yetu, ya ndani (ya nchi) na ya nje (nchi za
nje) utakuwa ni kujaribu, kiungwana, kuheshimu utu wa mtu.”
Alisema
Tanzania imeendelea na msimamo huo katika mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi
wa rangi na kwamba kwa muktadha huo Tanzania ilikuwa ni mwenyeji wa Kamati ya
Ukombozi wa Bara la Afrika (OAU) ikiwaunga mkono wapigania uhuru wa mataifa
mbalimbali ya Afrika.
Alisema
kwamba lakini pamoja na kupatikana kwa uhuru, mataifa hayo bado yanakabiliwa na
vikwazo vya kiuchumi na mazingira hatarishi kwa utu yanayokwamisha upatikanaji
wa maendeleo halisi. “Kwa hiyo tunatoa wito watu wajitawale wale ambao bado katika
mifumo ya ukoloni, na kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa kwa
mataifa ya Cuba na mengineyo.”
Alitumia
jukwaa hilo kuliarifu Baraza hilo juu ya uwepo wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa
na uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika nchini. “Novemba mwaka huu (2024),
Tanzania itafanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kisha kufuatiwa na uchaguzi wa
Rais na Wabunge Oktoba, 2025. Tunapojiandaa kwa matukio haya ya uchaguzi,
ningependa kuliarifu Baraza hili kuwa demokrasia, haki za binadamu, na utawala
wa sheria vitaheshimiwa, sambamba na maono ya Rais Samia kama ilivyoelezwa
katika falsafa ya 4Rs, ambazo ni upatanisho, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi
upya.”
0 Maoni