Katika siku za karibuni nchi yetu imeshuhudia kujirudia tena
kwa matukio ya kikatili ambayo yamehusisha kuripotiwa kwa vitendo vya utekaji,
utesaji na jana tukashuhudia tukio baya zaidi la mauaji ya kiongozi wa Chadema,
Ndugu Mohamed Ali Kibao.
Naungana na Watanzania wema wote kutoa mkono wa pole kwa
familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na viongozi na wanachama wa Chadema kwa
msiba huo wenye kuhuzunisha sana.
Nimetiwa moyo sana na taarifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan ambapo alieleza kusikitishwa
kwake na mauaji hayo na kutoa pole kwa wafiwa na wakati huo huo kuagiza
uchunguzi wa haraka wa tukio hilo na mengine kama hayo. Mheshimiwa Rais
hakuishia hapo tu bali alitoa ujumbe mzito kwa kusema kuwa: "Nchi yetu ni
ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza
haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii."
Namuunga mkono Rais wetu ambaye kwa nafasi yake ndiye
Mfariji Mkuu wa Taifa (Comforter-in-Chief) kwa kujitokeza na kuwafariji wafiwa
na Watanzania na kuwatangazia hatua za mara moja ambazo amezichukua ili
kukomesha ukatili huu.
Rais wetu siku zote ametuthibitishia kwa maneno na vitendo
kuwa kamwe hakubaliani na matendo ya aina yoyote ya kuumizana ama kutotenda
haki. Amejipambanua kuwa ni muumini thabiti wa haki kamili za kila binadamu.
Nikiwa raia wa Tanzania ambaye nimeitumikia nchi yetu katika
nafasi mbali mbali za uongozi na ambaye nililelewa katika Taifa linalothamini
tunu za utu na thamani ya ubinadamu wetu chini ya misingi ya uhuru na haki,
nawaomba Watanzania wenzangu sote tuungane kukataa kurudishwa kwenye zama za
giza ambapo utu na maisha ya mtu vilionekana havina thamani.
Naomba sote tuungane na Rais wetu kuhakikisha vitendo vya kishetani vya aina hii vinakomeshwa na havirejei tena katika nchi yetu. Sote tusimame pamoja kuona taifa letu linarudi katika misingi yake ya utu, uhuru na haki iliyojengwa na waasisi wake.
Rostam Azizi
9/9/2024
0 Maoni