Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amezitaka Mamlaka za Udhibiti na Ununuzi wa Umma Afrika Mashariki
kuzingatia weledi, maadili na uwajibikaji ili kuleta ufanisi uliokusudiwa.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo wakati akimwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa
Jukwaa la 16 la Ununuzi wa Umma kwa nchi za Afrika Mashariki na uzinduzi wa
Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) lililofanyika leo Septemba 9,
2024 jijini Arusha.
Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali zinatambua kwamba fedha
nyingi zinazotengwa kwenye bajeti kila mwaka zimekuwa zikitumika kupitia
ununuzi wa umma. Kwa kuzingatia hilo, Serikali imekuwa makini kuhakikisha kuwa
fedha hizo kupitia ununuzi wa umma zinapata usimamizi makini.
Ambapo kupitia
kifungu cha 7 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura ya 410 ya Mwaka 2023,
Serikali imeipa Wizara ya Fedha jukumu la kuhakikisha inaandaa Sera ya Taifa na
Mkakati wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ili kuhakikisha ununuzi na shughuli
zote zilizofunganishwa katika mnyororo wa ugavi zinazofanyika kwenye taasisi za
umma zinazingatia sera hiyo na mikakati itakayowekwa.
“Naomba Waziri wa
Fedha mlisimamie hili na haya ni maelekezo ya Mhe. Rais. Kupitia majukwaa
yaliyofanyika yote yametilia mkazo maadili, weledi, uwazi na uwajibikaji na
bila maadili wananchi hawezi kupata huduma, pia fedha nyingi zinazotengwa kwa
ajili ya wananchi kupata huduma zinaamriwa na kundi hili na kama hatuna taasisi
imara za ugavi na ununuzi hatutapata matokeo ya fedha na hatimaye umasikini
utaongezeka,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza “Nawaomba mnapojadili leo mkumbushane umuhimu
mkubwa wa kulinda taaluma yenu, ioneeni wivu isimamieni taaluma yenu akitokea
mtu anafanya vitendo visivyofaa mkemeeni. Jisimamieni wenyewe, asitokee mtu
katikakati ya manunuzi anataka kufanya vitendo visivyofaa, PPRA simamieni
vizuri jambo hili ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.”
Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali ya Tanzania
imefanya mageuzi makubwa ya kisheria katika ununuzi wa umma ambayo yalianza
mwaka 2001 kwa kutungwa kwa Sheria ya kwanza ya Ununuzi wa Umma. Baada ya
changamoto kadhaa, zilipelekea mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2004, na kuanzisha
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
“Serikali kupitia PPRA kama chombo cha Udhibiti wa Ununuzi
wa Umma ililenga kufanya mageuzi na kuboresha usimamizi wa ununuzi wa umma,
kuhakikisha thamani ya fedha, uwazi, na uwajibikaji, ufanisi na uadilifu katika
ununuzi na ugavi na kujenga uwezo katika ununuzi na ugavi katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania,” amebainisha Dkt. Biteko.
Ametaja maboresho yaliyofanywa na Serikali kuwa ni kuboresha
mfumo wa kisheria na kuweka miundo ya utawala, uboreshaji wa mifumo ya
kidijitali, kuajiri na kuwajengea uwezo wafanyakazi, kuboresha upatikanaji wa
zabuni kwa Watanzania ambapo ametolea mfano kuwa wazawa wakijengewa uwezo
wanaweza kufanyakazi vizuri hata nje ya nchi, pamoja na kuimarisha vita dhidi
ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Pia, Dkt. Biteko amesema kuwa Mamlaka zote za Ununuzi wa
Umma kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaoshiriki kwenye
Jukwaa hilo nao wana malengo yanayofanana na Tanzania.
“Kutokana na malengo ya uanzishwaji wa mamlaka hizi, natoa
wito kwa Mamlaka zote kuhakikisha kuwa mnasimamia malengo mliyoyaweka ili
kuhakikisha tija na ufanisi unapatikana katika usimamizi wa sekta hii ili
huduma kwa wananchi iendelee kupatikana kwa wakati na kwa ufanisi,” amebainisha
Dkt. Biteko.
Amesisitiza “Tunapotumia fedha za umma kununua bidhaa,
huduma au miradi katika nchi zetu, tunapaswa pia kufahamu hitaji la maendeleo
endelevu na ustawi wa ushirikiano baina ya nchi zetu za Afrika Mashariki. Hii
ina maana kwamba, mifumo yetu ya ununuzi kwa nchi za Afrika Mashariki inapaswa
kuhakikisha inajengwa kwa lengo la kuleta manufaa ya muda mrefu kwa wananchi
wetu.”
Akizungumzia mfumo wa NeST, Dkt. Biteko amefurahishwa na
mfumo huo kujengwa na vijana wa Kitanzania ambao nchi nchi nyingi za Afrika
Mashariki zimeanza kuutamani mfumo huo
ambao umekuwa na faida za kupunguza gharama za kufanya ununuzi kwa wazabuni wa
Serikali, kuondokana na matumizi ya karatasi, kuongezeka kwa kasi ya ununuzi
pamoja na kupunguza makosa katika ununuzi na kuboresha utoaji huduma kwa
wananchi.
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amewapongeza washiriki kutoka
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushiriki jukwaa hilo ambao
kupitia jukwaa hilo watapata fursa ya kubadilishana ujuzi na uzoefu pamoja na
kujadili masuala muhimu yanayohusiana na ununuzi wa umma kwenye nchi za Afrika
Mashariki.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad H. Chande
ameipongeza Serikali kwa kuendelea kufanya maboresho mbalimbali katika sekta
tofauti tofauti nchini ikiwemo sekta ya ununuzi wa umma ambao umeonesha kuwa na
tija katika sekta hiyo.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El Maamry
Mwamba amesema kuwa Jukwaa hilo linalenga kuwakutanisha wadau kuzungumzia
masuala ya ununuzi wa umma kwa manufaa
ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwa mwaka 2024 linafanyika
nchini Tanzania na kuandaliwa na Wizara ya Fedha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA),
Dkt. Leonada Mwagike ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa
kufanya maboresho makubwa katika sekta ya ununuzi wa umma na kuleta tija ya
kuongeza uwajibikaji ili kupata thamani halisi ya fedha inayoonekana.
Dkt. Mwagike ameahidi Mamlaka hiyo kuendelea kusimamia
utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na miongozo mbalimbali
inayotolewa na Serikali ili Watanzania wapate huduma bora.
“ Ili kuonesha ufanisi katika ununuzi wa umma Serikali
ilianza kutumia Mfumo wa Elektroniki wa Ununuzi wa Umma na baadae kujiunga
na Mfumo wa NeST na kuanza kutumika 2023
ambao umejengwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo eGA,” ameeleza
Dkt. Mwagike.
Amesema kuwa Mfumo huo unasomana na taasisi 17 ya mifumo ya
Serikali ikiwemo Benki Kuu, CRB, OSHA, TIRA, PeG kwa kuzingatia maelekezo
mahsusi ya Mhe. Rais ya kuhakikisha mifumo inasomana.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti ya Ununuzi wa Umma
(PPRA), Bw. Dennis Simba amesema kuwa majukwaa hayo hukutana kupitia nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo huwa na majadiliano na maazimio
na katika Jukwaa la 16 washiriki watapata fursa ya kuangalia utekelezaji wa
maazimio ya jukwaa la 15.
“Kupitia mada mbambali washiriki watapata fursa ya
kubadilishana uzoefu wa namna teknolojia inavyoweza kuongeza ufanisi katika
ununuzi wa umma na kusaidia nchi wananchama kuboresha ununuzi wa umma na
kushughulikia changamoto zilizopo katika ununuzi wa umma.” Amesema Bw. Simba.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA),
Mhandisi Benedict Ndomba ametaja moja ya jukumu la taasisi hiyo kuwa ni pamoja
na kusimamia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa umma
na inatambua kuwa ununuzi wa umma nchini ni eneo linalohitaji kusimamiwa vizuri
ili kuleta matokeo tarajiwa.
Mhandisi Ndomba ameongeza kuwa sambamba na kusimamia mifumo
mbalimbali ikiwemo Mfumo wa Uendeshaji Shehena na Mfumo wa Malipo Serikalini
(GePG), eGA inasimamia pia Mfumo wa ununuzi wa NeST.
“Hadi sasa mifumo 164 imeshaunganishwa na kuwezesha
kubadilishana taarifa ili kuongeza ufanisi, pia tunahamasisha taasisi zingine
zijuinge na mfumo huu ili kuongeza tija ya utendaji.” amemaliza Mhandisi
Ndomba.
Awali Dkt. Biteko amepokea tuzo aliyotunukiwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Samia Suluhu Hassan kwa jitihada
zake za kuboresha sekta ya ununuzi wa umma nchini. Aidha tuzo ingine imetolewa
kwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, Benki ya NMB, Stanbik na TCB,
Tanzanine Corporates, Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, Suma JKT, BRELA.
Taasisi zingine zilizopewa tuzo ni eGA, Shirika la Mzinga,
GPSA, TANESCO na Benki ya Maendeleo ya Kilimo, ISUZU, MSD, Kampuni ya Mtandao
wa Simu ya TIGO, Chuo cha Uasibu Arusha, Superdoll, TANROADS, CRDB, NSSF, TRA,
Ando, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, TMA, Clouds Media Group, AICC.
Jukwaa hilo la 16 limeongozwa na kauli mbiu inayosema “Utumiaji wa Mifumo ya Kielektroniki kwa Ununuzi wa Umma Endelevu”
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


0 Maoni