Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii
anaeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba asisitiza
matumizi ya sheria na kanuni katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za
uhifadhi.
Kamishna Wakulyamba ameyasema hayo leo Septemba 1, 2024
wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika ofisi za Makao Makuu ya TAWA
yaliyopo Mkoani Morogoro kwa lengo la kuongea na watumishi ili kuimarisha
utendaji kazi pamoja na kukagua maeneo ya kazi.
"Kama wahifadhi tunapaswa kufahamu sheria zote
zinazosimamia masuala ya uhifadhi zilizopo katika Taasisi zetu pamoja na za
Taasisi zingine za uhifadhi zilizopo ndani ya Wizara ya Maliasili na utalii,"
amesema Kamishna Wakulyamba.
"Pamoja na kufahamu sheria na kanuni zilizopo ndani ya
Wizara yetu, ni vyema kufahamu na kuzingatia sheria nyingine za Nchi ambazo
zinatuzunguka ili ziweze kutusaidia katika utekelezaji wa majukumu yetu mfano
sheria inayohusiana na ukusanyaji wa vielelezo
kuanzia kwenye ukamataji hadi kuwasilishwa mahakamani" ameongeza
Kamishna Wakulyamba.
Sambamba na hilo, Kamishna Wakulyamba amewapongeza Askari kwa
kazi nzuri wanazofanya na amewaasa kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu.
Awali, Kaimu Naibu Kamishna anayeshughulikia huduma za
uhifadhi, Mlage Kabange alitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali yanayosimamiwa
na TAWA huku akibainisha mafanikio na changamoto ya wanyama wakali na
waharibifu hususan katika Mikoa ya Kusini mwa Tanzania.
Katika ziara hii ya kikazi, Kamishna Wakulyamba aliambatana na Maafisa kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi , Mrakibu wa Polisi Joseph Jingu na Mrakibu wa Polisi Ocsar Felician waliopata fursa ya kutoa mafunzo maalum kwa watumishi wa TAWA.
Na. Joyce Ndunguru- Morogoro
0 Maoni