Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.
Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar bado inahitaji Wawekezaji zaidi kuja
kuwekeza nchini kupitia sekta mbalimbali.
Ameeleza kuwa zipo fursa nyingi za Uwekezaji Zanzibar ambazo
Wawekezaji wanaweza kuja kuwekeza katika nyanja mbalimbali na kuishauri Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuweka mkazo katika eneo
hilo.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo tarehe 09 Agosti 2024 wakati
alipokutana na Waziri Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliefika Ikulu
kujitambulisha baada ya kuteuliwa hivi karibuni.
Dk. Mwinyi amesema ni vema Wizara ijikite kutafuta
Wawekezaji wa kuja kuwekeza nchini pamoja na kunufaika Kidiplomasia na Mataifa
mengine.
Aidha, Dk. Mwinyi ameishauri Wizara hiyo kuzielekea nchi za
Asia na Mashariki ya mbali ambapo bado Zanzibar haijapata watalii pamoja na
wawekezaji wa kutosha kutoka Mataifa hayo.
Amesema Serikali imeendelea kuweka Mazingira mazuri ya
Uwekezaji na kuimarisha Miundombinu ili kuwavutia Wawekezaji kuja na kutumia
fursa hizo.
Naye Balozi Mahmoud amemuahakikishia Rais Dk. Mwinyi kuwa Wizara itafanya kila juhudi kuyafanyia kazi maelekezo yake kufungua milango mipya ya Uwekezaji.
0 Maoni