Kutokana na kuimarika kwa huduma bora za kibingwa na ubingwa
bobezi Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila imeendelea kuaminika na kuwa
kivutio cha matibabu nje na ndani ya nchi, hivyo kupelekea ongezeko la wagonjwa
wa nje (OPD) kutoka 600 kwa siku mwaka 2022 hadi kufikia wagonjwa 1117 mwaka
2024.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji
MNH-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi wakati akielezea mwenendo wa utoaji wa
huduma katika hospitali hiyo na kuongeza kuwa imani kwa wananchi kuhusu huduma
zinazotolewa Muhimbili Mloganzila imeongezeka sana ukilinganisha na miaka
miwili iliyopita.
Dkt. Magandi ameongeza kuwa sambamba na kuongezeka kwa
wagonjwa wa nje, idadi ya wagonjwa wanaolazwa imeongezeka pia kwa asilimia 70
hadi 80 kufikia 2024 ukilinganisha na asilimia 40 kwa mwaka 2022.
“Tumeendelea kuimarisha usimamizi wa huduma ikiwa ni pamoja
na kusikiliza maoni, ushauri, malalamiko ya wateja na kuyatafutia majawabu na
kuhakikisha kuwa wananchi wanapata mrejesho kwa wakati kitu ambacho kwa namna
moja ama nyingine kimeendelea kuimarisha uhusiano wetu na wale tunaowahudumia,”
ameongeza Dkt. Magandi.
Dkt. Magandi amebainisha kuwa ongezeko hilo limechagizwa pia
na kuongezwa kwa wigo wa kliniki za kuona wagonjwa wa nje ikiwemo kliniki za
mifupa, fiziotherapia pamoja na watoto ambazo pia zinafanyika siku za jumamosi
uanzishwa huduma za kiliniki za jioni.
Kwa mujibu wa Dkt. Magandi hospitali hiyo itaendelea kutoa huduma bora na zilizotukuka kwa wananchi na kufanya kila Mtanzania kutamani kufanyiwa uchunguzi na matibabu Muhimbili Mloganzila na hivyo kufikia lengo walilojiwekea la kuona wagonjwa wa nje 1,500 kwa siku siku za usoni.
0 Maoni