Polisi yatoa neno kutoweka kijana aliyechoma moto picha ya Rais

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa inayosambaa katika mitandoa ya jamii kuhusu kutoweka kwa kijana Shadrack Chaula [24] Mkazi wa Kijiji cha Ntokela Wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema limepokea taarifa za kutoweka nyumbani kwao kijana huyo Agosti 02, 2024 majira ya saa 8:30 mchana kutoka kwa baba mzazi wa kijana huyo aitwaye Yusuph Chaula [56] Mkazi wa Ntokela na limeanza kufanya ufuatiliaji na uchunguzi kuhusu taarifa hizo, hivyo linawataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki linapoendelea na uchunguzi.

Aidha, Kamanda wa Polisi Mbeya SACP Benjamin Kuzaga amesema polisi wanatoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa za mahali alipo kijana huyo aziwasilishe kwa njia iliyosahihi kwa viongozi wa Jeshi la Polisi ili kufanikisha kuwapata watu waliomchukua kijana huyo, lakini pia linaendelea kufanya uchunguzi wa kina na litatoa taarifa kwa umma.

Kijana huyo aliyechoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan, anadaiwa kutoweka wiki kadhaa tangu atoke gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa kosa hilo, na sasa Polisi mkoani Mbeya limewaomba wananchi kutoa ushirikiano katika kumtafuta kijana huyo.


Chapisha Maoni

0 Maoni