Vitongoji 68 vya Musoma Vijijini kunufaika na umeme wa REA

 

Wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini, Mbunge na viongozi wao mbalimbali wameishukuru Serikali ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua inzochukua za usambazaji wa umeme kwenye vitongoji 374 vya jimbo hilo.

Shukrani hizo zimetolewa na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo, wakati ambapo mradi wa usambazaji wa umeme vijijini wa (REA) katika vitongoji 68 ukitarajiwa kuanza jumatatu ya tarehe 12/08/2024.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini, imesema kazi ya usambazaji nguzo itaanza Jumatatu katika mradi huo utakaogharimu kiasi cha fedha shilingi bilioni 25.4 chini ya Mkandarasi Alpha TND Ltd.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa kuna mradi mwingine wa umeme katika vitongoji 15, ambao ni wa ahadi ya Wizara ya Nishati kwa wabunge wote wa mkoa wa Mara ambapo kila jimbo litasambaziwa umeme kwenye vitongoji 15.

Taarifa hiyo imesema Mkandarasi wa mradi huo Dieynem Co Ltd, anaendelea kufanya tathmini ya vitongoji 30 na kati ya hivyo 15 vitachaguliwa kusambaziwa umeme kwa kutumia fedha zitakazotolewa.

Jimbo la Musoma Vijijini lina Kata 21 zenye Vijiji 68 na Vitongoji 374, vijiji vyote 68 vina miundombinu ya kupokea na kusambaza umeme ambapo REA & TANESCO wanayo maombi ya kusambaziwa umeme kwenye vitongoji vyetu vyote.

Wakati huo huo, Prof. Muhongo ameridhia maombi ya wananchi wake ya kushirikia katika ujenzi wa Sekondari mpya za Jimbo la Musoma Vijijini na amepanga kufanya harambee za mfululizo kuanzia wiki Ijayo.

Chapisha Maoni

0 Maoni