Wafanyakazi wa Wakala wa Vipimo (WMA) Kitengo cha Bandari,
wamesema wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kufikia azma ya
Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwa na Tanzania ya Viwanda.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi, Meneja anayeongoza
Kitengo hicho, Alfred Shungu ameyasema hayo ofisini kwake alipokuwa akizungumza
na wanahabari, jana Agosti 21, 2024.
“Tunatambua kuwa Taifa linatutegemea hususani katika uhakiki
wa vipimo na upimaji wa mafuta yanayoingia nchini kuanzia melini, kwenye mita
na maghala ya kupokelea mafuta, hivyo tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa
weledi na uadilifu,” amesisitiza Shungu.
Akieleza kwa kina kuhusu majukumu ya Kitengo hicho, Shungu
amesema msingi wake ni kumlinda mlaji na muuzaji kwa kuhakiki utumiaji wa
vipimo sahihi katika biashara ya mafuta hapa nchini.
Aidha, amesema, majukumu yao pia yanalenga kuiwezesha
serikali kukusanya kodi kwa waagizaji wa mafuta kwa kuhakiki kiasi
kilichoagizwa na kampuni zinazoagiza mafuta jamii ya petroli na mafuta ya kula
kutoka nje ya nchi.
Shungu amedadavua zaidi kuwa majukumu ya WMA Kitengo cha
Bandari katika Meli yanahusisha kuhakiki kiasi cha mafuta yanayowasili nchini
kwa kulinganisha na nyaraka za Meli za kuagiza mafuta pamoja na kukagua vipimo
vyote vinavyotumika kupimia mafuta.
Upande wa Mita, amesema WMA inawajibika kuhakiki mfumo wa
upimaji wa mafuta kwa kutumia kipimo kilichohakikiwa na Wakala hiyo. Pia, WMA
hupaswa kuweka kumbukumbu ya vipimo na takwimu za matokeo ya upimaji kwa
kulinganisha melini na kwenye maghala na kutoa ushauri wa kitaalamu ikibainika
kutofautiana.
Aidha, katika maghala, Shungu ameeleza kuwa wajibu wa WMA ni
kukagua vipimo vinavyotumika kupima mafuta kwenye matenki, kupima na kuchukua
takwimu za kiasi cha mafuta yaliyopo kwenye matenki kabla ya kupokea mzigo
pamoja na kuweka alama kwenye matenki yanayopokea mzigo na yasiyopokea mzigo.
Majukumu mengine katika matenki ni kupima na kuchukua
takwimu za kiasi cha mafuta yaliyoingia kwenye matenki baada ya kupokea mzigo,
saa 24 baada ya mafuta kutulia pamoja na kukokotoa kiasi cha mafuta yaliyoingia
katika kila ghala kwa Meli nzima.
Amesema baada ya hapo, WMA huandaa taarifa ya upimaji na kusambaza kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Mojawapo ya vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari
vilivyopo nchini. Wakala wa Vipimo, Kitengo cha Bandari hufanya kazi ya
kuhakiki Pampu zinazotumika kujazia gesi ili kumlinda mlaji/mnunuzi na muuzaji,
wote wapate faida stahiki. Habari pamoja na picha na Pendo Magambo- WMA.
0 Maoni