Afisa Mhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania- TAWA Winniefrida Kweka amesema Wanyamapori waliopo nchini wana
mchango mkubwa katika Sekta ya Utali kwakuwa huchangia zaidi asilimia 17 katika
pato la Taifa.
Winniefrida ametoa kauli hiyo Agosti 04, 2024 alipokuwa
akitoa elimu ya uhifadhi kwa mamia ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma waliotembelea
bustani ya wanyamapori hai iliyopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na
Utalii kwenye maonesho ya NaneNane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni
Mkoani humo.
"Wanyamapori wanachangia sana kwenye Sekta ya utalii
kwa zaidi ya asilimia 17 za pato la nchi, asilimia zote hizi zinachangiwa na
utalii unaohusisha wanyama wa porini," amesema.
Winniefrida amesema kutokana na faida zitokanazo na
wanyamapori hao kwa nchi, TAWA inatumia maonesho hayo kuwaelimisha watanzania
wote kuachana na mitazamo hasi kuwa wanyamapori ni viumbe wasio na mchango
chanya kwa Taifa.
Aidha Mhifadhi huyo amesema kutokana na changamoto
inayoletwa na baadhi ya wanyamapori wakali na waharibifu kama vile mamba,
tembo, fisi na wengine, TAWA imekuwa ikielimisha umma juu ya mbinu rafiki za
kuweza kuishi na wanyamapori hao na
kuendelea kubaki salama kwa kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na
wanyamapori hao.
Vilevile Winniefrida
amebainisha kuwa chanzo kikubwa cha migongano baina ya wanyamapori hususani
mamba na binadamu ni pale ambapo binadamu anapokuwa anahitaji mahitaji yake
sehemu ambapo wanyamapori hao wapo (majini).
Amesema kufuatia changamoto hiyo Serikali kupitia Taasisi
zake za kiuhifadhi imekuwa ikitoa elimu ya kujilinda dhidi ya athari zinazoweza
kusababisha na wanyama hao ikiwa ni pamoja na kusaidia katika ujenzi wa
vizimba vya mfano ili kuepusha madhara
ya wanyamapori hao.
Winniefrida ametoa wito kwa
wavuvi kufanya shughuli zao za
uvuvi kwa njia zilizo sahihi na kuepuka kutega mitego yao ya Samaki sehemu
ambazo mamba walipo na kuachana na dhana iliyojengeka miongoni mwao kuwa palipo
na mamba ndipo pana samaki wengi.
Maonesho ya mwaka huu yaliyobeba kauli mbiu isemayo "Chagua viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa maendeleo endelevu ya Kilimo, mifugo na uvuvi" yalianza tarehe Agosti 01, 2024 na yanategemewa kufika kilele Agosti 08, 2024.
Na. Beatus Maganja- Dodoma
0 Maoni