Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuhakikisha
watanzania wanapata Taarifa na kuibua fursa mbalimbali kupitia Idara na Taasisi
zake maonesho ya Wakulima Wavuvi na Wafugaji "Nanenane" pamoja na
kuwajengea uwelewa wananchi juu ya Utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi
wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).
Akiongelea ushiriki wa
mradi wa REGROW katika maonesho hayo makubwa yanayofanyika kitaifa
Jijini Dodoma, Afisa Ufuatiliaji na
Tathmini wa Mradi Bw. Michael Kalaghe, amesema lengo ni kutoa elimu kwa
umma juu ya utekelezaji wa mradi na kuanika fursa na manufaa yaliyopo kwa
watanzania kupitia REGROW.
Bw. Kalaghe ameongeza kuwa ushiriki wa mradi huo Nanenane
licha ya kutoa elimu kwa umma, pia ni sehemu muhimu ya kupokea maoni kutoka kwa
watu na wadau mbalimbali juu ya utekelezaji
wa mradi.
Aidha, Mzee Joshua Chavala ameipongeza Serikali kwa kazi
kubwa inayofanya katika kuinua utalii Kusini kupitia Mradi REGROW kwani licha
ya maelezo aliyopata kupitia Maonesho ya Nanenane, ameshuhudia kupitia vyombo
vya habari namna wananchi wanavyonufaika kupitia Benki za Kijamii
"COCOBA'.
Naye Bi. Neema Adrian Makazi wa Babati, licha ya kuipongeza
Serikali kwa juhudi kubwa za kuwainua wananchi kiuchumi kupitia Mradi wa REGROW
ameishauri kuupeleka Mradi huo utekelezwe kote nchini ili wananchi wafaidike na
fedha za Miradi kwa jamii kama wanavyonufaika sasa na mradi huo wananchi
waishio Kusini mwa Tanzania.
Mradi wa REGROW unaotekelezwa Kusini mwa Tanzania umelenga kuimarisha Usimamizi wa Maliasili, Kuwainua wananchi kiuchumi pamoja na kuchechemua utalii kwenye vivutio vilivyopo Kusini mwa Tanzania.
Na. Sixmund Begashe- Dodoma
0 Maoni