Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt.
Emmanuel John Nchimbi ameiagiza Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa Vitambulisho
vya Uraia (NIDA) kwa wananchi wa Ngara, mkoani Kagera, wanaokidhi vigezo.
Nchimbi ameyasema hayo jana Agosti 7, 2024 alipokuwa
akizungumza na maelfu ya wananchi wa Mji wa Ngara, katika Uwanja wa Posta,
akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Kagera, baada ya Mbunge wa Jimbo
la Ngara Mhe. Ndaisaba George Ruhoro kuwasilisha kilio hicho kwenye mkutano
huo.
Mapema pia kabla ya mkutano wa hadhara huo, Balozi Nchimbi
alitoa maelekezo kuhusu suala hilo la upatikanaji wa vitambulisho vya NIDA,
aliposimama kuwasalimia wananchi wa
Kijiji cha Kumunazi alipokuwa njiani
akitokea Biharamulo, kueleeka Ngara.
Akiwa ameambatana na wajumbe wa Sekretarieti ya CCM Taifa
katika ziara hiyo; Ndugu Issa Haji Usi Gavu, Ndugu Amos Gabriel Makalla na
Ndugu Rabia Hamid Abdallah, Balozi Nchimbi ameielekeza Wizara hiyo kuchukua
hatua haraka ili changamoto hiyo imalizwe.
Amesema hata utaratibu wa kuruhusu watu kuazimana
vitambulisho vya NIDA kwa shughuli mbalimbali ni jambo hatari, linaloweza
kusababisha uhalifu.
"CCM itasimamia ili kuhakikisha suala hilo linafanyiwa kazi na kasi ya utoaji wa vitambulisho vya NIDA inapatikana," amesema Dk. Nchimbi.
0 Maoni