Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) limeendelea kuwa kivutio baada ya kuongezwa zao jipya la utalii tofauti na ilivyokuwa katika matamasha ya miaka ya nyuma ya Kizimkazi.
Zao hilo jipya la Utalii wa Nyuki (Api-tourism)
linalohusisha kudungwa na nyuki, na mazao ya nyuki yaliyoongezewa thamani kama vile asali,
chavua, karanga za asali, maziwa ya nyuki ambavyo watu hutumia kama dawa na
virutubisho katika mwili limeonekana kuwa kivutio sambamba na wanyamapori hai
kama vile simba, chui, fisi, pundamilia na pofu.
Zao jipya la Utalii wa Nyuki (Api-tourism), linalojumuisha
shughuli za kudungwa na nyuki na mazao ya nyuki yaliyoongezewa thamani kama
vile asali, chavua, karanga za asali, na maziwa ya nyuki ambavyo hutumika kama
dawa na virutubisho vya mwili vimekuwa kivutio kikubwa sambamba na wanyamapori
hai kama vile simba, chui, fisi, pundamilia, na pofu.
Akiongea mara baada ya kuwapokea viongozi na wageni
mashuhuri bandani hapo jana Agosti 20, 2024, Ephraim Mafuru, Mkurugenzi Mkuu wa
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) amesema ikiwa ni siku moja kabla ya kuazimisha
Siku ya Utalii katika Tamasha la Kizimkazi ameshuhudia umati mkubwa ukifika
kudungwa na nyuki tofauti na zamani.
“Mapema mwaka huu Tanzania na China zilitiliana saini
Itifaki ya kuuza Asali ya Tanzania nchini China na kutoa wito kwa watanzania
kuchangamkia fursa ya kuzalisha asali yenye ubora kwa wingi ili kuinua vipato
vyao na uchumi wa taifa kwa ujumla.”
“Lakini mbali na hayo tumewaleta wananchi zao jipya la
utalii wa nyuki, tumekuja na mzinga uliojaa nyuki, tunawadungisha watu, na mimi
mwenyewe leo nimedungwa mara mbili, sijavimba na wala mkono hauniumi, na kama
unavyoona mwitikio ni mzuri wananchi wanachangamkia fursa ya kudungwa, tena
huduma hii tunaitoa bure jambo ambalo huwezi kupata sehemu nyingine,” anasema.
Brenda Mwakipesile ni moja kati ya wahifadhi wanaodungisha
nyuki mamia ya wananchi wanaoendelea kumiminika kutembelea banda kuu la Wizara
ya Maliasili na Utalii anasema kuwa, utalii huo mpya nchini umekuwa kivutio kwa
wananchi wengi kutokana na kuwa ni tiba ya asili inayosaidia kuimarisha kinga
ya mwili dhidi ya maradhi mbalimbali na ustawi wa afya kwa ujumla.
Miongoni mwa wananchi waliojitokeza ni mhamasishaji maarufu
na machachari wa mitandaoni Dotto Keto, maarufu kama Dotto Magari ambaye mara
baada ya kudungwa na nyuki aliwaasa wananchi kuja kujionea maajabu ya utalii
huo mpya wa nyuki, ili kupata fursa ya kujidunga bure na nyuki ndani ya viwanja
vya Kizimkazi, akisema kuwa hii ni nafasi adimu na yenye faida nyingi kwa afya.
“Jamanii njoo Kizimkazi muone utalii wa nyuki, ma’nake nyuki
tunawaogopa lakini hapa kuna binti jasiri, anawashika anawatuliza, nimedungwa
safi kabisa, huu utalii wetu kiboko! Mkurugenzi Mafuru upewe maua yako,”
anasema.
Tamasha la Kizimkazi lilianza mwaka 2015 ikiwa ni sherehe ya kumuaga Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais John Magufuli na baada ya kuteuliwa alikutana na wananchi wa Kizimkazi na kufanya sherehe ya kumuaga mwaka 2016 iliyojulikana kwa jina la Samia Day na ilipofika nwaka 2017 jina likabadilishwa na kuwa Kizimkazi day.
0 Maoni