WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania watoe
taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapokuta kuna bidhaa zisizo rasmi zimeagizwa
kutoka nje, zinazalishwa au zinasambazwa nchini.
Ametoa wito huo Bungeni leo (Alhamisi, Agosti 29, 2024)
wakati akijibu swali la Mbunge wa Hai, Saasisha Mafue kwenye kipindi cha
maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua Serikali
inatoa kauli gani ili kudhibiti tabia ya vijana kulewa sana nyakati za mchana
hali ambayo inasababishwa na uingizaji holela wa pombe kali.
“Serikali inao utaratibu wa kutambua uzalishaji na uingizaji
wa vileo nchini ambao unadhibitiwa kwa kutoa vibali vya biashara kwa
wasambazaji. Vilevile inaendelea kutoa elimu juu ya madhara ya ulevi kupitiliza
ili kuwalinda vijana wetu.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuwahamasisha vijana wajiunge kwenye vikundi ili wafanye
shughuli za ujasiriamali. Utaratibu huu umesaidia vijana wetu kupata kipato
chao binafsi na familia zao.
Ili kudhibiti hali hiyo, Waziri Mkuu amesema Serikali
inaendelea kutoa elimu ili vijana wengi waingie kwenye shughuli za ujasiriamali
na kuimarisha sheria za waagizaji, wauzaji na wasambazaji ili kuhakikisha kila
kinachoingizwa nchini kinakidhi mahitaji ya afya ya Watanzania.
“Jamii itusaidie kutambua utengenezaji wa bidhaa usiokuwa
rasmi ambao haujapata vibali rasmi kwani unachangia kutengeneza bidhaa zenye
vileo vikali. Nitoe wito kwa taasisi zote zinazojihusisha na masuala ya vijana
ziendelee kutoa elimu ya ujasiriamali, kuwafundisha maadili mema vijana wetu na
kuwapa stadi za maisha.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema kuwa huduma za afya
nchini zimeimarishwa sana na uwekezaji mkubwa umefanywa kiasi kwamba hatua za
awali za utambuzi wa mama mjamzito zinaweza kubaini aina ya ulemavu kwa mtoto
aliyenaye tumboni.
“Tafiti zetu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa hatua za
awali zinaweza kubaini ulemavu na kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza ulemavu
kwa zaidi ya asilimia 80. Kwa maana hiyo, uwekezaji uliofanywa kuanzia ngazi ya
zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, za mkoa, za kanda na Taifa si tu
kuamua hospitali moja katika mkoa iwe inatoa huduma kwa walemavu bali kwenye
vituo vyote ambavyo Serikali imeviboresha.”
Ametoa wito kwa akinamama wahudhurie kliniki mapema ili
wapate elimu na kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara hadi atapojifungua.
Alikuwa akijibu swali la Khadija Taya (Viti Maalum) ambaye alitaka kujua ni upi mkakati wa Serikali wa kuweka vituo katika kila mkoa ambavyo vitatoa huduma za kunyoosha viungo kwa watoto wanaozaliwa na ulemavu.
0 Maoni