Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA)
imetekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati mkoani Simiyu ikiwemo ujenzi wa
madaraja na barabara katika wilaya, halmashauri, kata na vijiji vya mkoa huo.
Hayo yameelezwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi
Gaston Paschal wakati wa mahojiano maalum yaliyofanyika mkoani humo, mwishoni
mwa wiki.
“Katika utekelezaji wa miradi yetu, tuna miradi ya
kimkakati, ambayo inagusa wananchi moja kwa moja, na unakuta ilikuwa ni kilio
cha siku nyingi katika maeneo yao,” amesema Mhandisi Gaston.
Amesema, Wilaya ya Busega kulikuwa na changamoto kati ya
Kata ya Mwamanyili na Kata ya Nyaluhande kutokana na mto uliotenganisha kata
hizo mbili.
Aidha, TARURA imefanikiwa kujenga daraja la Mwamanyili lenye
upana wa mita 20, na kuwezesha wananchi kupita kutoka kata moja kwenda nyingine
bila changamoto yoyote.
Kwa upande wa Wilaya ya Bariadi, TARURA imekamilisha ujenzi
wa daraja la Mwadobana lenye urefu wa Mita 36, ambalo limeunganisha kata nne
katika wilaya hiyo.
Kwa upande wa Wilaya ya Itilima, TARURA inatekeleza ujenzi
wa barabara ya KM 5.2 ambayo inagharimu shilingi bilioni 3.4, ujenzi huo
unatumia teknolojia mbadala ya Ecoroads.
“Barabara hii inakwenda Hospitali ya Wilaya ya Itilima,
hivyo itakapokamilika itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Wilaya ya
Itilima, hasa kwa wagonjwa wanaokwenda kupata matibabu katika hospitali ya
wilaya,” amesema Mhandisi Gaston.
Ameendelea kusema kuwa, kwa Wilaya ya Maswa kulikuwa na
shida ya maji kufurika na tope katika eneo la Maswa Mji, ambapo mwaka jana
TARURA imefanikiwa kujenga barabara ya lami KM. 1 na kuweka taa katika eneo
hilo korofi.
“Upande wa Meatu
tunajenga daraja la Mwanzagamba kwa kutumia teknolojia rahisi, lenye upana wa
Mita 25, ambalo limekamilika na linaunganisha kata tatu,” amesema Mhandisi
Gaston.
Amesema, miradi hiyo imebadilisha muonekano wa mtandao wa
barabara mkoani humo, ambapo kulikuwa na barabara nzuri zinazopitika asilimia
22, kwa sasa zimefikia asilimia 46 na barabara zisizoridisha zimepungua kutoka
asilimia 36 hadi asilimia 18. Vilevile madaraja yameongezeka kutoka madaraja
101 mpaka madaraja 140, sawa na ongezeko la asilimia 38.
Mkoa wa Simiyu una wilaya tano, ambazo ni Busega, Bariadi, Maswa, Itilima na Meatu, ambapo Mtandao wa barabara unaohudumiwa na TARURA katika mkoa huo ni KM 4,163.38.
0 Maoni