Serikali imesema imejidhatiti kuendelea kufanyia maboresho
sheria za ulinzi wa Watoto ili ziweze kuendana na wakati huu wa sasa kwa
maslahi mapana ya kuwalinda Watoto.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb), alipokuwa akichangia Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali za Ulinzi wa Mtoto wa Mwaka 2024.
“Sisi kama Serikali ni wajibu wetu kuhakikisha tunaleta
Bungeni sheria za Watoto ili zifanyiwe maboresho,” Mhe. Chana amesisitiza.
Kuhusu hoja ya namna ya kudhibiti mitandao ya kijamii na
uharibifu wa mitandao hususan kwa Watoto, Mhe. Chana ameishukuru Wizara ya
Habari, Mawasiliano na Teknolojia kwa kuendelea kudhibiti baadhi link zenye
maudhui potofu kwa ajili ya kuwalinda Watoto.
Aidha, amesema pamoja na mambo mengine Serikali imeendelea
kuboresha muhimili wa mahakama zikiwemo mahakama za watoto na kupunguza
mlundikano wa kesi, kuboresha majengo ya mahakama ambapo kuna mahakama katika
wilaya takribani 137 nchini ambako kwenye mahakama zote kuna mahakama za
Watoto.
Pia, amefafanua kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba
maamuzi ya kesi za Watoto yanatoka haraka katika mahakama kwa sababu serikali
inafahamu watoto wana haki ya elimu huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuteua Majaji
na Mahakimu ambao wanaosimamia kesi hizo za Watoto.
Katika hatua nyingine, Mhe. Chana amesema Serikali imefunga video conference inayowezesha kesi kuendeshwa wakati watuhumiwa/wahalifu wakiwa bado magerezani na pia kwa kuona umuhimu wa elimu kwa Watoto Serikali imejipanga kufanya maboresho kwa kutumia e-learning wakati watoto wakiwa katika vifungo vyao ili kuwepo na haki ya wao kupata elimu.
0 Maoni