Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff ameelezea maeneo manne ya vipaumbele vya TARURA katika kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara za Wilaya nchini.
Mhandisi Seff aliyasema hayo wakati wa uwekaji jiwe la
msingi wa ujenzi wa daraja la mto Hurui wilayani Kondoa mkoani Dodoma.
Alisema kuwa kipaumbele cha kwanza ni matengenezo ya
miundombinu ya barabara ili kulinda uwekezaji ambao tayari umeshafanyika, ikiwa
ni kuendelea na matengenezo hata pale barabara na madaraja yanapokamilika ili
miundombinu hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu.
Alieleza kuwa kipaumbele kingine ni kuondoa vikwazo kwenye
mtandao wa barabara za Wilaya ili ziweze kupitika katika misimu yote ya mvua,
mojawapo ya kazi ya kuondoa vikwazo ni pamoja na kujenga barabara kwa kutumia
zege, kuweka makalavati na vivuko maeneo yote korofi ili hadi kufikia mwaka
2025/26 asilimia 85 ya mtandao wa barabara za Wilaya uweze kupitika nyakati
zote.
"Mtandao wetu una zaidi ya Km. 144,000 lakini
rasilimali fedha tunazopata bado ni kidogo, hivyo tunajitahidi kadri
tunavyopata rasilimali fedha tunaondoa vikwazo ili barabara zetu ziweze
kupitika nyakati zote," alisema Mhandisi Seff.
Vile vile aliongeza kusema kuwa Wakala unatumia teknolojia
mbadala pamoja na malighafi za ujenzi zinazopatikana maeneo ya kazi ikiwemo
mawe katika ujenzi na matengenezo ya barabara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa
gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kutunza mazingira.
Pia, alisema wanazipandisha hadhi barabara kutoka udongo
kuwa changarawe lakini kutoka changarawe au udongo na kuwa barabara za lami kwa
kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kijamii.
"Tunahudumia zaidi ya Km. 144,000 ya mtandao wa
barabara lakini zaidi ya Km. 100,000 ni barabara za udongo, hizi ndio zina
changamoto kubwa msimu wa mvua kwani
maeneo mengi yanakuwa hayapitiki na kutokea taharuki ndio sababu tunajitahidi
kadri rasilimali fedha tunazopata kuhakikisha kwamba tunaondoa vikwazo vyote
ili barabara ziweze kupitika misimu yote ya mvua," aliongeza.
0 Maoni