Makumbusho inayotembea yaipamba Nanenane Dodoma

 

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi yake ya Makumbusho ya Taifa nchini, inafanya kazi kubwa ya kurithisha Urithi wa Malikale na Utamaduni kwa kizazi cha sasa hususani kinachotembelea Maonesho ya 30 ya Wakulima Wavuvi na Wafugaji "Nanenane" yanayofanyika Kitaifa Jijini Dodoma.

Katika maonesho hayo, wananchi wengi wametokea kupendezwa na kuipongeza Wizara hiyo kwa ushiriki wa Taasisi ya Makumbusho kwa kuwa inatoa nafasi kwa wazazi na watoto kujifunza kuhusu urithi adhimu na adimu wa kihistoria na Utamaduni ambao si rahisi kwa kizazi cha sasa kujifunza  kutokana na mlipuko wa utandawazi.

Akiwa ameambatana na wanafunzi zaidi ya 30, Mwl. Moses wa Shule ya Mazengo Dodoma, amesema kuwa, wanafunzi wa Shule hiyo wamefurahi sana mafundisho walioyapata katika Gari maalumu la Makukumbusho, kwani licha ya kujifunza historia ya nchi, wamepata pia kujifunza matumizi ya teknolojia ya asili kwenye eneo la uandaaji wa chakula, zana za asili na malezi ya watoto kwa ujumla.

Naye Mwl. Florida Lwabe wa Shule ya Msingi Nzasa, Dodoma ameelezea furaha yake baada ya wanafunzi wa Shule anayofundisha kushiriki program maalumu ya Uzalendo, Mila na Desturi katika Makumbusho inayotembea na kuiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuwafikia wanafunzi mashuleni kupitia Makumbusho hiyo.

Pamoja na mambo mengine katika Banda la Maliasili na Utalii, wananchi wanaofika hapo wanapata nafasi ya kugundua fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya Misitu na Nyuki, Wanyamapori, Miradi mbalimbali ya Uhifadhi na Utalii ukiwemo mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).

Na, Sixmund Begashe - Dodoma

Chapisha Maoni

0 Maoni