Wadau wa uchaguzi kutoka mikoa ya Mwanza na Shinyanga kesho
watakutana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuzungumzia Uboreshaji wa Darftari
la Kudumu la Mpiga Kura katika mikoa yao wakati wa mzunguko wa tatu wa
uboreshaji.
Akizungumzia maandalizi ya Mkutano huo, Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Bw. Kailima Ramadhani
amesema mikutano hiyo na wadau wa uchaguzi inalenga kupeana taarifa mbalimbali
za maandalizi kwa ajili ya kuanza rasmi kwa zoezi la uboreshaji wa Daftari.
“Lengo hasa la kukutana na wadau hawa ni kupeana taarifa za
uwepo wa zoezi hili na kuwapitisha katika vifaa na mifumo ya uandikishaji
pamoja na kuona namna zoezi litakavyofanyika vituoni. Aidha,tutapeana taarifa
juu ya maandalizi ya Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, na maandalizi hayo pamoja na mambo mengine
yanajumuisha uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura, uboreshaji wa
majaribio, ununuzi wa vifaa na ushirikishwaji wa wadau kama ambavyo itafanyika
kesho katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga,”amesema Kailima.
Amewataja wadau watakao shiriki mikutano hiyo ni pamoja na
Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia,
Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na
Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu,
Wanawake na Wazee wa Kimila na wote ni kutoka mikoa husika.
Aidha, katika
mikutano hiyo kutakuwa na mada ya
Mkurugenzi wa Uchaguzi mada
itakayozungumzia uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Wataalamu wa
TEHAMA watawapitisha kwenye mfumo wa uandikishaji na vifaa vitakavyotumika.
Katika Mada ya Mkurugenzi wa Uchaguzi itagusia masuala
mbalimbali ikiwepo uzinduzi wa zoezi la Uboreshaji wa Daftari, Uboreshaji wa
Daftari,Wasio na sifa za kuandikishwa,Idadi ya wapiga kura wanaotarajiwa
kuandikishwa, Maandalizi ya uboreshaji wa Daftari, Mafunzo kwa watendaji wa
uboreshaji, Ushirikishwaji wa wadau, Taasisi na Asasi pamoja na Mchango wa
wadau katika kufanikisha zoezi la uboreshaji.
Tume tayari imeanza zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura ambapo uzinduzi ulifanyika mkoani Kigoma tarehe 20 Julai, 2024
na mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Kassim Majaliwa Majaliwa (MB). Uzinduzi huo ulienda sambamba na kuanza kwa
mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kwenye mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na
Katavi.
Aidha, mzunguko wa pili wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaendelea sasa katika mikoa ya Kagera na Geita ambapo uboreshaji ulianza tarehe 5 hadi 11 Agosti, 2024.
0 Maoni