Katika hatua kubwa inayotarajiwa kuleta mapinduzi katika sekta ya ufugaji nyuki, Serikali ya Tanzania imefanikiwa kusaini makubaliano na Serikali ya China, kuruhusu uuzaji wa asali ya Tanzania kwenye soko la China.
Makubaliano haya yanafuatia jitihada za muda mrefu za
kuhakikisha bidhaa za asali kutoka Tanzania zinapata nafasi ya kuuzwa katika
soko kubwa zaidi duniani.
Akizungumza leo Agosti 15,2024 jijini Dar es Salaam katika
hafla ya uwekaji saini itifaki ya kuuza asali ya Tanzania nchini China, Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dustan Kitandula, alieleza kuwa kufunguliwa
kwa soko la China ni matokeo ya mawasiliano ya muda mrefu kati ya nchi hizi
mbili, ambayo yalianza mwaka 2018.
"Huu ni ushindi
mkubwa kwa wafanyabiashara wa asali nchini. Sasa wanaweza kuuza bidhaa zao
kwenye soko lenye mahitaji makubwa zaidi duniani," alisema Mhe. Kitandula.
Mhe. Kitandula pia alibainisha kuwa, kwa mujibu wa
makubaliano hayo, wafanyabiashara wa asali watatakiwa kuhakikisha kuwa
wanakidhi vigezo vya kimataifa vya usalama wa chakula na afya, ikiwa ni pamoja
na kusajili makampuni yao kwenye Mifumo ya Kimataifa ya Udhibiti wa Afya na
Usalama wa Vyakula; Afya ya Mimiea; na Ulinzi wa Mazingira.
Anasema ili kufanikisha hilo, Serikali kupitia Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeanzisha dawati maalum la kusaidia
wafanyabiashara hao kujisajili kwa njia ya kidigitali. Hata hivyo amesema hadi
sasa ni kampuni 12 tu ndizo zimejisajili kwenye mfumo huo, hivyo ametoa rai kwa
kampuni ambayo bado hazijasajiliwa kujisajiliwa.
Pamoja na hayo amempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa
kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha rasilimali zilizopo, ikiwemo misitu,
nyuki na wanyamapori zinaendelea kuhifadhiwa kwa ajili ya matumizi ya sasa na
vizazi vijavyo.
"Jitihada zake za uhifadhi wa rasilimali hizi, Rais Dk.
Samia ameendelea kutangaza na kuvutia wawekezaji katika sekta yetu ya ufugaji
nyuki. Uongozi wake umekuwa chachu ya kuimarika kwa Sekta ya Maliasili na
Utalii, huku akilenga sio tu kutunza mazingira na bionuwai, bali pia kuboresha
maisha ya Watanzania kupitia miradi mbalimbali.
“Ufugaji nyuki ni sekta muhimu ya kiuchumi inayoathiri moja
kwa moja maisha ya wananchi, hasa wale wanaoishi karibu na maeneo
yaliyohifadhiwa. Sekta hii imekuwa chanzo cha ajira kwa takribani watu milioni
mbili, hususan vijana na wanawake, na inachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha
hali ya maisha ya Watanzania.
“Tanzania ina maeneo makubwa ya misitu yenye ukubwa wa hekta
milioni 48.1, ambayo inawezesha uzalishaji mkubwa wa asali. Ingawa nchi ina
uwezo wa kuzalisha tani 138,000 za asali kwa mwaka, kwa sasa inazalisha tani
33,276, sawa na asilimia 24.1 ya uwezo huo. Pamoja na changamoto hizo, Tanzania
inashika nafasi ya kwanza kwa uzalishaji wa asali Afrika Mashariki na SADC, na
nafasi ya pili barani Afrika, ikionesha umuhimu wa sekta hii kwa uchumi wa
taifa,” anasema Mhe. Kitandula.
"Ufugaji nyuki ni moja ya shughuli ya kiuchumi
inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi wa kawaida hususan wale wanaoishi
karibu na maeneo yaliyohifadhiwa. Shughuli hiyo imekuwa ni chanzo muhimu cha
ajira, hasa kwa vijana na wanawake, ambapo takribani watu milioni mbili nchini
wamejiajiri kupitia ufugaji nyuki,"amesema.
Anaongeza kuwa, ingawa Tanzania inazalisha kiwango kikubwa
cha asali, ni asilimia tano tu ya asali hiyo inayouzwa nje ya nchi, kutokana na
masharti mbalimbali ya kibiashara. Asali na nta ya Tanzania huuzwa hasa katika
masoko ya Ulaya, Marekani, na Mashariki ya Kati, na mauzo haya huipatia nchi
wastani wa dola milioni 12.9 za Kimarekani kila mwaka, sawa na shilingi bilioni
30.58.
Mhe. Kitandula alisisitiza kuwa Serikali imeweka mikakati
madhubuti ya kuongeza uzalishaji na ubora wa asali, huku ikilenga kuongeza
mauzo nje ya nchi. Hii inajumuisha utekelezaji wa Mpango wa Udhibiti wa Mabaki
ya Kemikali na Mfumo wa Ufuatiliaji wa Ubora wa Asali, ambao unalenga
kuhakikisha asali ya Tanzania inakidhi viwango vya kimataifa na inavutia wateja
wa kimataifa, hivyo kuimarisha ushindani na kuongeza Pato la Taifa.
Sambamba na hilo anasema Serikali imeweka mazingira rafiki
kwa wafugaji nyuki na wafanyabiashara kwa kutoa msamaha wa VAT kwenye vifaa na
mashine zinazohusiana na ufugaji na usindikaji wa mazao ya nyuki. Msamaha huu,
ulioanzishwa kupitia Sheria ya Msamaha wa Kodi Na. 10 na Sheria ya Fedha Na. 6
ya mwaka 2024, unalenga kuongeza uzalishaji na mauzo ya asali nje ya nchi.
“Serikali imeanzisha utaratibu maalum kupitia Wizara ya Maliasili
na Utalii kwa ajili ya kupata msamaha huu, na inahimiza wawekezaji kuchangamkia
fursa hii,” anasema.
Kwa upande wake Waziri na Katibu wa Kamati ya CPC ya Utawala Mkuu wa Forodha ya Watu wa Jamhuri ya China Yu Jianhua amesema soko la China lina zaidi ya watu bilioni 1.4, na kila mwaka nchi hiyo inaagiza zaidi ya tani milioni 38 za asali. “Hii inamaanisha kuwa kuna fursa kubwa kwa Tanzania kupata mapato makubwa kupitia biashara ya asali na bidhaa nyingine za nyuki,” anasema.
0 Maoni