Ziara ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi
Dkt. Emmanuel John Nchimbi, inayoendelea katika mikoa ya Kusini, akianzia
Mtwara na sasa yuko Lindi, imewahamisha viongozi waandamizi wa vyama vya ACT
Wazalendo, CUF na Chadema walioamua kujiunga CCM leo, wakisindikizwa na mamia
ya wanachama waliorejesha kadi zao za vyama vya zamani kwa kasi kubwa kwenye
mkutano wa hadhara.
Katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa
Mpilipili, Lindi mjini, ukiwa ni mwendelezo wa ziara ya Balozi Nchimbi,
amewapokea viongozi hao waandamizi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha ACT
Wazalendo Mkoa wa Lindi na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mchinga Ndugu Hamidu
Bobali akiambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Wanawake wa ACT
Wazalendo Lindi Mjini Bi. Hawa Kipara, Meneja Kampeni wa Wabunge ACT Wazalendo
Lindi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana CUF Lindi Issa Sapanga, Katibu wa ACT
Wazalendo Mkoa wa Pwani, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Mchinga, Mwenyekiti wa
Wanawake Chadema Lindi Mjini pamoja na Wanachama 250 wa ACT Wazalendo.
Wakati akikabidhi kadi yake ya ACT na kujiunga CCM, Ndugu
Bobali amesema;
“Nimeishi miaka 20 nje ya CCM ambako niliaminiwa sana katika
ngazi tofauti ndani ya CUF na ACT Wazalendo hadi kuwa Waziri Kivuli wa Maji
lakini nikiri niliyokuwa yanapigania Jemedari Samia ameyafanya kwa nguvu kubwa
hivyo sina jinsi isipokuwa kujiunga CCM na kumuunga mkono. Kule upande wa pili
tulikokuwa ametupiga kwenye mshono, hakuna tena agenda. Sasa hakuna kingine
zaidi ya kazi nzuri za Dkt Samiana wenzangu hawa sasa tupo tayari kumsaidia.”
Naye Balozi Nchimbi akiwapokea wanachama hao wa vyama mbalimbali wakiongozwa na ACT Wazalendo amesema “karibuni huku wanachama wote ni sawa na mtapata ushirikiano mkubwa sana kuanzia sasa na kikubwa mmesema mmerudi sababu ya mambo makubwa yaliyofanywa na Dkt Samia nawapongeza kwa kuliona hilo mapema sasa tukaifanye Lindi ya kijani.”
0 Maoni