WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Iringa na
Watanzania kwa ujumla waingie kwenye kilimo cha Parachichi kwa kuwa zao hilo
linachochea ukuaji wa uchumi.
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali
ilikuwa ikitafuta masoko kwa ajili ya maparachichi yanayozalishwa nchini badala
ya kutegemea nchi jirani pekee.
“Tumeshapata soko la moja kwa moja kwa ajili ya maparachichi yetu nchini
China na India na tumegundua ya kwetu yana thamani kubwa na ubora wa hali ya
juu ukilinganisha na maparachichi kutoka nchi nyingine.”
Ametoa wito huo jana jioni (Jumapili, Julai 7, 2024) wakati
akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali mara baada ya kukagua mradi wa
kitalu cha miche bora ya parachichi unaomilikiwa na kikundi cha vijana cha
Chilongola, kilichopo kata ya Upendo, Mafinga Mjini, mkoani Iringa.
Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania waingie kwenye
mpango wa kuzalisha miche ya zao hilo ili kuongeza idadi ya uzalishaji wa
maparachichi. “Maparachichi yetu yana ubora mkubwa. Na hii ni baada ya kupima
udongo nchini kote na kubaini kuwa tuna maeneo yenye udongo unaofaa kwa kilimo
hiki,” amesema.
Akizungumzia suala la barabara kama lilivyowasilishwa na
wana kikundi hao, Waziri Mkuu amesema miundombinu ya barabara za kwenda
mashambani linaratibiwa vizuri na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini
(TARURA) pamoja na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).
Kuhusu suala la kukosa mlango wa malimbichi bandarini,
Waziri Mkuu Majaliwa amesema analipokea suala hilo na kuahidi kuwa
atalifuatilia.
Mapema, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema
Serikali imeshasaini mkataba na kampuni ya Afac Engineering ambayo itajenga
kiwanda cha kusindika maparachichi katika eneo la Nyololo ambapo katika awamu
ya kwanza, sh. bilioni 3.4 zitatumika.
“Wana-Mufindi ni watu wanaolima sana. Mbunge wenu amesimamia
ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan ya kujenga kiwanda cha
kusindika maparachichi. Mkataba ulisainiwa na kabla ya Ijumaa ijayo,
tutamkabidhi eneo mkandarasi ili aanze kazi,” alisema.
Akielezea kuhusu kusuasua kwa zao la chai, Naibu Waziri huyo
alisema kuwa Serikali inatambua changamoto iliyokuwepo ya kiwanda cha DL lakini
tayari Serikali imeshafanya maamuzi ya kukinunua kiwanda hicho na kukikabidhi
kwa wakulima wadogo wadogo wa chai wa Mufindi ili wakiendeshe kupitia ushirika
wao.
Kuhusu soko la mahindi, Naibu Waziri Silinde aliwataka
wananchi hao wajiandae kuuza mahindi kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
(NFRA) kuanzia Julai 10, mwaka huu na kuahidi kuwa bei itakuwa nzuri. Hata
hivyo, hakutaja bei hiyo.
Akifafanua zaidi, alisema: “Kutoka Zambia, tumepokea oda ya
tani 650,000 za mahindi. Nchi jirani ya Congo (DRC) nao wametaka tani 500,000
lakini wanataka tuwape tani 200,000 za awali. Kwa hiyo, jiandaeni kuuza mahindi
kuanzia tarehe 10 Julai, 2024.”
Naye, Mkurugeni wa kampuni ya Chilongola Agroforestry &
Livestock, Andrew Salika alisema kikundi chao kilianza mwaka 2020 kwa kuzalisha
miche 9,000 lakini hivi sasa wana miche 250,000 iliyo tayari kwenda sokoni.
“Lengo letu ni kuongeza idadi ya miche bora ambapo mahitaji ni miche 730,000
kwa msimu mmoja,” alisema.
Wakati huohuo, Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi alisema
mji wa Mafinga ni miongoni mwa miji iliyopo kwenye mradi mkubwa wa maji wa miji
28 nchini lakini mradi umefikia asilimia 18 tu kutokana na kusuasua kwa kasi ya
mkandarasi.
Aliiomba Serikali isimamie kwa karibu ujenzi wa barabara ya
Mafinga hadi Mgololo kwa kuwa wilaya ya Mufindi inabeba uchumi wa mkoa mzima wa
Iringa. “Barabara hii ikiisha, itarahisisha sana usafirishaji wa mazao ya
wakulima na kuwa mkombozi wa wananchi wengi,” alisema.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa,
alimweleza Waziri Mkuu kwamba wilaya hiyo ina ekari 800,000 ambazo ni miti tupu
na kati ya hizo, ekari 500,000 ni za miti ya kupandwa. Alisema wilaya hiyo ina
viwanda 40 vya kuchakata mazao ya miti pamoja mazao ya kilimo kama chai na
pareto.
Aliishukuru Serikali kwa kuwapelekea umeme ambapo hadi
vijiji vyote 312 vya wilaya hiyo vimepata umeme na kuongeza kuwa hivi sasa
wamejipanga kukamilisha uwakaji umeme vitongojini. “Tuna vitongoji 612, ambapo
vitongoji 412 vimeshapata umeme na kati ya 200 vilivyobakia, 107 vipo kwenye
mpango wa kupatiwa umeme mwaka huu,” alisema.
Waziri Mkuu amefuatana pia na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile.
0 Maoni