Unyama mwingi Mnyama akizindua jezi Unyamani Hifadhi ya Mikumi

 

Timu ya Simba SC imeendelea kuweka historia ya kuwa kinara wa ubunifu wa kutangaza vivutio vya utalii nchini baada ya kuzindua kwa staili ya aina yake jezi zake mpya za msimu 2024/25 katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi Mkoani Morogoro.

Kama hiyo haitoshi uzinduzi huo mbali ya kutangaza hifadhi hiyo kubwa ya nne nchini yenye ukubwa wa kilomita za mraba 3,230 pia Simba SC wamepiga ndege wawili kwa jiwe moja kwa kutangaza pia usafiri wa treni mpya ya umeme ya mwendokasi ya SGR ambayo walitumia kusafiri nayo.

Huu ni mwendelezo wa Simba SC kutangaza utalii ambapo katika msimu uliomalizika walitumia ubunifu kama huo wa kutangaza utalii kwa kutumia kibegi kilichopanda mlima mrefu kuliko yote Afrika, Mlima Kilimanjaro na kuzindua jezi zake kwenye kilele cha mlima huo.

Katika uzinduzi jana Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Augustine Masessa alisema amefurahishwa na kitendo ambacho kimefanywa na timu ya Simba SC, kwani ni moja ya njia inayotumika kuitangaza hifadhi hiyo ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na timu hiyo kutazamwa na mashabiki na watazamaji zaidi ya milioni 50 ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

“Uongozi wa Hifadhi ya Mikumi kwa ujumla wake tumefurahishwa sana na tukio hili la kihistori kwani limeweza kuitangaza vema hifadhi yetu, naushukuru uongozi mzima wa timu ya Simba SC, naziomba timu nyingine nazo zifanye hivi,”alisema Masessa.

Pamoja na pongezi hizo Kamishna Masessa aliongeza kwa kusema kuwa kitendo kilichofanywa na timu ya Simba SC kimenogesha juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suhulu Hassan kwa kutangaza vivutio mbalimbali hasa Hifadhi za Taifa zilizopo hapa nchini ikiwemo ya Mikumi.

Kamishna Masessa alisema kuwa tukio lilofanywa na timu ya Simba SC mbali na kuitangaza hifadhi ya Mikumi, pia limeonyesha wazi kuwa ndani ya hifadhi hiyo kuna huduma mbalimbali ikiwemo suala zima la michezo ya aina mbalimbali ambapo watu wanaweza kwenda kufurahia mandhari ya hifadhi hiyo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa timu ya Simba SC, Iman Kajula alisema waliamua kwenda kuzindua jezi zao mpya hifadhi ya Mikumi kwani wao wamekuwa mstari wa mbele kutangaza utalii hapa nchini lakini pia walikwenda kukutana na wajina wao ambao ni simba wa sharubu.

Aidha, Kajula aliwapongeza mashabiki wa timu hiyo waliyojitokeza katika uzinduzi wa jezi zao ikiwa ni pamoja na wiki yao ambayo kilele chao kitakuwa Agosti 3 mwaka huu ambapo aliwataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kutembelea hifadhi hiyo.

Afisa Habari wa timu hiyo, Ahamed Ally alisema kuwa wameamua Hifadhi ya Taifa Mikumi kuzindua jezi zao mpya kwani hifadhi hiyo ni moja ya hifadhi maarufu hapa nchini lakini pia kuonana na wajina wao kwa jina la Simba wa Mikumi na kwamba kupitia tukio lao hilo la kihistoria umaarufu wa Simba wa Kariakoo na wa Mikumi utaongezeka zaidi hali itakayochochea utalii katika hifadhi hiyo.

Januari mwaka huu Simba SC, pia wakati ikishiriki Michuano ya Mapinduzi, ilitangaza kusaidiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika kutangaza utalii kwa kutembelea maeneo ya vivutio vya utalii pamoja na kuvaa jezi zilizoandikwa Visit Zanzibar.


Chapisha Maoni

0 Maoni