MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inatumia
maonesho ya 48 ya kimataifa ya kibiashara yanayoendelea Jijini Dar es Salaam
kuhamasisha Umma wa watanzania wawekezaji na wageni kutoka mataifa mbalimbali
kuwekeza katika maeneo inayoyasimamia huku ikijinasibu kuwa na fursa lukuki za
uwekezaji.
Akiongea na wageni waliotembelea banda la TAWA lililopo
ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii Afisa utalii Daud Tesha amesema
TAWA ina uwanda mpana wa fursa za uwekezaji unaotoa mwanya kwa wawekezaji wa
aina mbalimbali kuwekeza katika Taasisi hiyo.
Akizitaja fursa hizo Tesha amesema yapo maeneo mengi
yanayohitaji wawekezaji na uwekezaji katika Taasisi hiyo kama vile maeneo ya
utalii wa picha kwenye maeneo ya hifadhi za Wanyamapori, maeneo ya kihistoria
yenye Utalii wa kiutamaduni, eneo la uwekezaji mahiri (Special Wildlife
Investment Concession Areas - SWICA), Uwindaji wa Kitalii na Ufugaji wa
Wanyamapori.
"TAWA imetenga maeneo kadhaa Kwa ajili ya kufanyika
shughuli za utalii wa picha kutokana na ikolojia na aina ya vivutio vilivyopo
katika maeneo hayo ikiwemo Pori la Akiba Mpanga/Kipengere eneo ambalo lina
maporomoko ya maji zaidi ya 10 ambayo hutoa burudani safi kwa watalii,"
amesema Daud Tesha.
"Maeneo mengine
ni Pori la Akiba Wamimbiki, Tabora ZOO,
Ruhila ZOO , Makuyuni Wildlife Park ambapo wananchi wanakaribishwa kuwekeza
kwenye miundombinu ya Utalii ikiwemo kujenga Kambi za Kulala wageni
(Campsites), Hosteli, Loji na maeneo ya mapumziko mafupi kwa watalii (Picnic
Sites),” ameongeza.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja ametumia
fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wote kutembelea banda la TAWA Ili kupata
maelezo ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi hiyo.
"Kama kauli mbiu ya Maonesho haya inavyosema kuwa
Tanzania ni Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji, nitumie fursa hii kuwaambia
watanzania wote kuwa TAWA ni Taasisi sahihi kwa biashara na uwekezaji kwani
inatoa fursa za uwekezaji wa aina mbalimbali kama vile ujenzi wa loji, kumbi za
mikutano katika maeneo yetu, kambi za watalii, michezo ya watoto lakini kama
haitoshi mwekezaji anaweza akatumia fursa ya kuwekeza katika mashamba ya
wanyamapori, bustani za wanyamapori nk," amesema Maganja.
"Kwahiyo hii ni fursa adhimu Kwa wawekezaji wote
kutembelea banda letu ili waweze kupata ufafanuzi wa fursa mbalimbali za
uwekezaji zilizopo katika taasisi yetu," ameongeza Maganja.
Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja, akiongelea fursa za uwekezaji na kuwakaribisha wananchi wote kutembelea banda la TAWA katikaMaonesho ya 48 ya Kimataifa ya Kibiashara (Sabasaba).
Maonesho haya yenye Kauli Mbiu "Tanzania ni Mahali Salama Pa Biashara na Uwekezaji" yameanza 28 Juni, 2024 na yanatarajiwa kufikia tamati 14 Julai, 2024.
0 Maoni