Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, Mhe.George Simbachawene amesema
siasa za kisasa ni kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na sio kuzungumza
maneno matupu huku akiwataka wananchi kuwapuuza wale wote wanaokejeli maendeleo
yaliyofanywa na Serikali jimboni kwake na nchini kote kwa ujumla.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo wakati akizungumza na
wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kibakwe iliyopo
Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma ambapo amesema
Kibakwe ya sasa ni tofauti sana na ile ya miaka kadhaa
iliyopita, huku akitolea mfano kuwa mwaka 2005 jimbo hilo lilikuwa dhoofu sana
kwenye huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji, umeme pamoja na barabara.
"Kibakwe ninayoiona leo inafurahisha sana, tumetekeleza
Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo na kwa kiasi kikubwa sana kwani
utitiri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa mnaiona wenyewe," amesema
Mhe. Simbachawene.
Akizungumzia mradi wa miundombinu ya barabara jimboni humo,
Mhe. Simbachawene amesema Kibakwe ya sasa imefunguka huku akitaja uwepo wa
barabara za lami pamoja na utengenezaji wa barabara kila kona katika Jimbo hilo
ukiwa unaendelea.
"Leo tumekagua ujenzi wa barabara ambapo mmeshuhudia
wenyewe uwekaji wa lami kuelekea Shule ya Sekondari Kibakwe pamoja na
kuelekea Kanisa Katoliki ukiwa unaendelea, hizi ndizo siasa za kileo,"
amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Ameongeza kuwa taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa
barabara ya kiwango cha lami kutokea Mpwapwa hadi Kibakwe unaendelea.
Aidha, Mhe. Simbachawene amezungumzia mradi mwingine wa
ujenzi wa Chuo cha VETA unaoendelea katika Jimbo hilo la Kibakwe utakaogharimu
kiasi cha shilingi bilioni 1.6 hadi kukamilika kwake ambapo amesema ukikamilika
utatatua changamoto ya ajira kwa vijana nchini, hususan katika Jimbo hilo la
Kibakwe.
Amefafanua kuwa, chuo hicho cha VETA mara baada ya
kukamilika kwake kitasaidia kuwaandaa vijana kujiari badala ya kusubiri
kuajiriwa huku akisema vijana watakaohitimu chuoni hapo watachochea kukua kwa
uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, huku akisema katika Jimbo hilo
kila Kata ina shule zaidi ya moja
ya ya Msingi na Sekondari.
Vile vle Mhe.Simbachawene ameongeza kuwa huduma za afya
katika Jimbo la Kibakwe zimeboreshwa sana
tofauti na mwanzo ambapo amesema
Kituo cha Afya cha Kibakwe ambacho kwa sasa kina hadhi sawa na Hospitali ya
Wilaya ya Mpwapwa kwani kina vifaa vya kisasa ikiwemo majokofu ya kuhifadhia
miili, vifaa vya huduma za dharula
pamoja na huduma ya afya ya mama na mtoto.
Wakati huo huo, Mhe. Simbachawene ametambua jitihada za mtu
mmoja mmoja zilizofanywa na wananchi wa Kibakwe na kuchangia maendeleo ikiwemo
ujenzi wa nyumba za kisasa katika jimbo
hilo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kibakwe, Mhe. David Chisanza amemuelezea Mhe. Simbachawene kuwa ni Kiongozi wa mfano ambaye katika kipindi chote cha uongozi ameendelea kuzigusa familia za wana Kibakwe kwa namna tofauti kimaendeleo.
0 Maoni