WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema maendeleo yaliyopo
nchini hivi sasa yametokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya Serikali na sekta
binafsi.
“Maendeleo tunayoyaona nchini kwetu katika kila sekta
yanategemea mchango wa Serikali pamoja na sekta binafsi. Dhamira na maono ya
Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuimarisha sekta binafsi ili ihuishwe na
kuwa mshindani katika kuleta maendeleo makubwa kwa nchi yetu,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumanne, Julai 23,
2024) wakati akizungumza na wadau wa sekta binafsi nchini kwenye ufunguzi wa
maadhimisho ya Wiki ya Sekta Binafsi Tanzania kwa mwaka 2024 yaliyofanyika
Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam.
Wiki ya Sekta Binafsi Tanzania inaenda sambamba na
maadhimisho ya miaka 25 ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Amezitaka wizara na taasisi za Serikali ziendelee kupokea
maoni ya sekta binafsi na kuhakikisha yanazingatiwa katika marekebisho ya sera
na sheria za biashara ili kuondoa vikwazo vya urasimu na kuboresha taratibu za
usajili na uendeshaji wa biashara nchini kwa kuwezesha upatikanaji wa vibali na
leseni kwa haraka na kwa urahisi.
Pia amezitaka wizara zinazohusika na viwanda, biashara na
uwekezaji zihakikishe zinabuni mbinu za kukuza na kusaidia biashara ndogo na za
kati (SMEs). “Wekeni mazingira mazuri ya upatikanaji wa mikopo nafuu, mafunzo
na ufikiaji wa masoko ili kusaidia biashara ndogo na za kati kukua na kuchangia
katika uchumi. Biashara hizi ni sehemu muhimu ya kuimarisha sekta binafsi.”
Akielezea jitihada ambazo zimechukuliwa ili kukuza sekta
binafsi na uwekezaji, Waziri Mkuu amesema Serikali imeimarisha mazingira ya
biashara kwa kufanya marekebisho katika sera na sheria za biashara ili kuondoa
vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara na wawekezaji.
“Hatua hizi zimejumuisha kuboresha taratibu za usajili wa
biashara, kupunguza urasimu, na kuongeza uwazi, kutoa fursa za uwekezaji katika
sekta mbalimbali kama vile kilimo, nishati, miundombinu, utalii, viwanda na
kuanzisha maeneo maalum ya uwekezaji.”
Amesema Serikali
imewekeza katika miundombinu ya usafirishaji, nishati, maji na mawasiliano
ambayo ni muhimu kwa shughuli za uwekezaji na biashara. “Hatua hii inalenga
kuimarisha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje,”
amesema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzugumza na washiriki wa
hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)
Jenista Mhagama amempongeza Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuasisi falsafa mpya ya kushirikiana na
Sekta binafsi ikiwemo kuondoa ukiritimba wa mawazo.
“Rais wetu yeye anaamini na anakiri katika dhana ya
kusikiliza sauti na mawazo ya wengine ili kuweka mazingira bora ya mahusiano
kati ya Sekta binafsi na Serikali.”
Amesema kuwa kupitia falsafa hiyo imeshuhudiwa Rais Dkt. Samia akiendesha vikao vya kubadilishana mawazo mara kwa mara na makundi tofauti ya sekta binafsi yaliyojikita katika sekta mbalimbali kwa kusikiliza changamoto, kujifunza mafanikio na kutengeneza mfumo thabiti na sahihi wa kusonga mbele kwa manufaa ya pande zote mbili.
Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe
alisema katika mwaka huu wa fedha, wizara hiyo imeweka vipaumbele sita ambavyo
vinalenga kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuchochea ukuaji wa
uchumi.
Kwa upande wake, Mweyekiti wa TPSF, Angelia Ngalula, alisema
kuwa wanatamani kuona Tanzania inakuwa kitovu cha Afrika kutokana na rasilmali
ilizonazo. “Pia tunatamani kuona biashara nyingi zinarasimishwa na wigo wa
walipakodi unaongezwa,” alisema.
Alisema wakati TPSF inaanzishwa, ilikuwa na wanachama 33 lakini kwa sasa imefikisha wanachama zaidi ya 500 ambao wanajumuisha vyama vya wafanyabiashara na makampuni makubwa.
0 Maoni