Rais Samia kumpokea Rais Nyusi wa Msumbiji

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,  anatarajia kumpokea Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi Julai 02, 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam. Rais Nyusi anatarajia kuwasili nchini leo jioni ambapo atafanya ziara ya Kiserikali ya siku tatu.

Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa B. Nyanga imeseama Rais Samia na mgeni wake Rais Nyusi watashiriki mazungumzo ya pamoja ambayo yatajikita katika sekta ya biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama na kisha kushuhudia uwekaji saini wa makubaliano katika sekta mbalimbali za ushirikiano.

Ziara hii itaendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria, kidugu na kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na Msumbiji ambao uliasisiwa na viongozi wetu; kiongozi wa kwanza wa chama tawala cha nchi hiyo (FRELIMO), Hayati Eduardo Chivambo Mondlane na Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere, imesema taarifa hiyo.

Rais Nyusi pia anatarajia kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) siku ya tarehe 03 Julai, 2024 ambapo ataambatana na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan kabla ya kuondoka nchini Julai 04, 2024.

Chapisha Maoni

0 Maoni