Naibu Katibu Mkuu - Utalii, Nkoba Mabula ameitaka Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti pamoja na TANAPA kwa ujumla kuendelea kutoa elimu ya Utalii wa ndani kwa jamii na ubunifu utumike ili kuongeza idadi ya watalii hususani watalii wa ndani.
Mabula ametoa wito huo katika ziara ya kikazi Serengeti
yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo pamoja na shughuli za Uhifadhi na
Utalii katika Hifadhi hiyo mkoani Mara.
"Muendelee kutoa elimu ya Utalii wa ndani katika vyuo, shule za Sekondari na msingi, walimu na
taasisi. Kidogo kidogo wataelewa na kuanzisha programu maalum za usafiri ili
waweze kumudu".
Aidha, Mabula
amewapongeza Maafisa na askari kwa weledi mkubwa katika kazi licha ya
changamoto zinazoikabili Hifadhi na kuahidi kuwa changamoto zote amezipokea na
atazifikisha kwa viongozi wa juu .
Awali, akiukaribisha ugeni huo kwa niaba ya Kamishna wa
Uhifadhi - TANAPA, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Massana
Mwishawa alisema, Hifadhi ya Taifa Serengeti imekuwa ikipokea wageni wengi kwa
kipindi chote cha mwaka, hivyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali hususani
changamoto ya miundombinu.
"Changamoto kubwa katika Hifadhi hii ni miundombinu ya
barabara na baadhi ya viwanja vya ndege kwani ndege, magari na wageni wanazidi
kuongezeka siku hadi siku."
Naibu Kamishna, Mwishawa alibainisha ni faraja kubwa kwa
viongozi kufika na kufanya ziara, kuona uhalisia wa utendaji kazi kutoka juu
mpaka ule wa chini na kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii
kwa jitihada kubwa inayoendelea kuzifanya katika kuboresha miundombinu
mbalimbali pamoja na miradi ya maendeleo
katika hifadhi za Taifa.
Naibu Katibu Mkuu Nkoba Mabula anaendelea na ziara ya
kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika hifadhi ya Taifa Serengeti ambayo
ni hifadhi bora barani afrika kwa miaka mitano
mfululizo ikiwa ni maarufu zaidi duniani kwa msafara wa nyumbu wanaohama
kila mwaka pamoja na uwepo wa wanyama wengi wadogo kwa wakubwa yaani “The Big
five”.
Na. Brigitha Kimario- Serengeti
0 Maoni