Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kugawa mabomu
baridi yapatayo 700 kwa ajili kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu
wilayani Nachingwea.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa kata za
Mkoka na Kilimarondo wilayani Nachingwea, ikiwa ni muendelezo wa ziara ya
kuwaeleza wananchi juu ya jitahada zinazifanywa na serikali kudhibiti
changamoto ya wanyama wakali na waharibifu.
Aidha, Mhe. Kitandula alisema kuwa serikali itaendelea
kutumia mbinu mbalimbali za kisayansi ikiwemo matumizi ya ndege nyuki, uvishaji
wa mikanda ya mawasiliano na visukuma mawimbi, na matumizi ya helikopta katika
kukabiliana na changamoto ya wanyama wakali na waharibifu. Sambamba na hatua
hizo, serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa askari wanyamapori wa vijiji (VGS)
pamoja na kuwapatia vitendea kazi ili kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na
hivyo kuzuia wanyama hao wasiendelee kuleta uharibifu na usumbufu kwa wananchi.
Vilevile Mhe. Kitandula alikemea tabia ya baadhi ya viongozi
wa vijiji kuruhusu mifugo kuingia kwenye maeneo ya hifadhi vitendo ambavyo
vinasababisha uharibifu wa ikolojia ya wanyama ikiwemo tembo na kuwafanya
kutafuta mazingira mengine rahisi kwao kuishi.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mhe. Mohamed Moyo
akimkaribisha Naibu Waziri kuongea na wananchi alisema kuwa serikali ya wilaya
itaendelea kutilia mkazo suala la kuwaondoa wafugaji walioko kwenye maeneo ya
hifadhi na kuwapeleka kwenye maeneo yaliyotengwa kwa kufuata Mpango wa Matumizi
Bora ya Ardhi.
Kwa upande wake mbunge wa Nachingwea Mhe. Dr. Amandus
Chinguile akiwasilisha salama za wananchi wa wilaya ya Nanchingwea alitumia
fursa hiyo kuipongeza wizara pamoja na Taasisi ya Usimamizi wa wanyamapori
(TAWA), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), na Wakala wa huduma za Misitu
(TFS) kwa kazi kubwa sana wanayoifanya ya kudhibiti ujangili wa mazao ya misitu
na kupambana na wanyama wakali na waharibifu.
“Pamoja na kazi kubwa inayofanywa na askari hao lakini hawatoshi kwa kuwa makundi ya wanyama wakali na waharibifu ni makubwa, hivyo sio rahisi kwa vijana waliopo kuweza kuwamudu kwa wakati mmoja,” alisema Mhe. Chinguile.
0 Maoni