Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda
amepata nafasi ya kukutana na ujumbe wa makamanda walioongozana na melivita ya
matibabu ya Jeshi la Ukombozi la watu wa China 'Peace Ark' ofisini kwake Upanga
jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo naye.
Katika mazungumzo hayo Kiongozi wa Ujumbe huo Rear Admiral
HongBo Ying amelishukuru Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa mapokezi
makubwa pamoja na ushirikiano walioupata tangu walipowasili hapa nchini tarehe
16 Julai mwaka huu wakiwa na meli vita ya matibabu.
Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda
amesema JWTZ linapoelekea kuadhimisha kilele cha miaka 60 tangu kuanzishwa
kwake, linashirikiana na Jeshi la China katika matibabu na mazoezi ya medani.
Amewasihi watanzania kujitokeza kwa wingi kwenye tiba ili
kupimwa afya zao pamoja na kupata matibabu bila malipo kwani JWTZ limeamua
kushirikiana na Jeshi la China ikiwa ni muendelezo wa ushirikiano kuelekea
kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya JWTZ.
Matibabu hayo bila malipo yataanza rasmi tarehe 18 Julai
hadi 23 Julai mwaka huu.
Tangu kuanzishwa kwa JWTZ miaka 60 iliyopita jeshi limekuwa na ushirikiano wa kidugu na Jeshi la China baada ya kuasisiwa na Marais wa kwanza wa nchi hizi mbili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mao Zedong.
0 Maoni