Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka watendaji wa
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani Tabora na Katavi kuwa na
ushirikiano kati yao, Serikali, Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mafunzo ya siku
mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa
Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na
Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo Julai 9 na 10,2024 Mkoani Tabora.
Mafunzo kama hayo yamefunguliwa pia Mkoani Katavi na Mjumbe
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe.
Asina Omari na yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye
mikoa hiyo unaotarajiwa kufanyika tarehe 20 hadi 26, 2024.
“Matokeo bora ya zoezi hili yanategemea uwepo wa ushirikiano
mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji, Serikali, Vyama vya Siasa na wadau
wengine wa uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegele.
Jaji Mwembegele amewasihi watendaji hao kuwa na ushirikiano
mzuri na wa karibu na Tume wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao na ikiwa
wanahitaji ufafanuzi au maelekezo yeyote, wasisite kuwasiliana na Tume.
Aidha, Jaji Mwambegele amesema wakati wa uboreshaji wa
Daftari mawakala wa Vyama vya Siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha
wapiga kura jambo ambalo litasaidia kuleta uwazi katika zoezi hilo.
“Mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika
hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima. Mawakala hao
hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao
vituoni,”alisema Jaji Mwambegele.
Katika hatua nyingine amesema Tume imetoa vibali kwa Asasi
za kiraia 157 kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura na waangalizi wa zoezi la
uboreshaji 33 watakao tazama zoezi la uboreshaji.
Jaji Mwambegele amesema Tume inasisitiza kwa Maafisa
Waandikishaji kuwa, wanapofika katika maeneo yao, wapewe ushirikiano kwa kuwa
ni wadau muhimu.
Mafunzo hayo yanahusisha namna ya ujazaji wa fomu pamoja na
kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura (Voters Registration System - VRS) ili
waweze kupata uelewa wa pamoja utakaowapa fursa ya kutumia kwa ufasaha mfumo
huo pamoja na vifaa vingine vya kuandikisha wapiga kura.
“Mafunzo haya, yanawajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa
Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata kisha nao watatoa mafunzo hayo kwa
Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi ambao ndio
watahusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni,” alisema Jaji Mwambegele.
Aidha, Maafisa TEHAMA watapatiwa mafunzo maalum ya jinsi ya kukabiliana
na changamoto mbalimbali za kiufundi (Troubleshooting) endapo zitajitokeza
wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.
Mapema kabla ya kuanza mafunzo hayo, washiriki walikua kiapo
cha kujitoa uanachama na kile cha kutunza siri.
Tume imetangaza uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika Julai 20, 2024 mkoani Kigoma ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na kauli mbiu ya uboreshaji ni “Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura ni Msingi Wa Uchaguzi Bora.”
0 Maoni