Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Hassan
Abbasi amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa kupitia kampuni yake ya SUMA -JKT kwa
kufikia zaidi ya asilimia 90 kukamilisha ujenzi wa nyumba 2,500 zinazojengwa katika Kijiji cha Msomera
wilayani Handeni mkoani Tanga.
Dkt Abbasi ametoa kauli hiyo katika ziara aliyoifanya
Kijijini hapo tarehe 8 Julai, 2024 na kusema kazi iliyofanywa na jeshi hilo ni
kubwa na ya kizalendo hivyo zoezi lililobaki sasa ni kuendelea kuelimisha,
kuhamasisha na kuhamisha wananchi wanaoendelea kujiandikisha kuhama kwa hiyari
katika eneo la tarafa ya Ngorongoro.
Amesema kuwa ujenzi wa nyumba hizo unaenda sambamba na
ujenzi wa miundombinu mingine ya huduma za kijamii ambapo wizara za kisekta zimekuwa zikiendelea kujenga miundo mbinu
hiyo ikiwemo shule,usambazaji wa
umeme,maji ,mawasiliano na huduma zote za msingi katika Kijiji hicho.
Katibu mkuu huyo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana namaono yake kaatika
utekelezaji wa mradi huo ambao kukamilika kwake kutatimiza utekelezaji wa
malengo ya serikali ya kuhakikisha kila
mtanzania anakuwa na maisha bora.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Handeni mheshimiwa Albert
Msando amemshukuru Dkt Abbasi kwa ziara hiyo na kusema kuwa itaongeza ari kwa
wizara nyingine za kisekta kuongeza kasi katika ukamilishaji wa miradi yote
muhimu na hivyo kuifanya Msomera kuwa Kijiji cha mfano.
Mheshimiwa Msando amesema kuwa uendelevu wa mradi huo
unaondoa propaganda za watu wachache kwamba wananchi wanaohamishwa kutoka
Ngorongoro kwenda katika Kijiji hicho wanaondolewa kwa nguvu na kutelekezwa
jambo ambalo halina ukweli wowote.
Akizungumzia kuhusu suala la kuhamisha watu kwa hiyari
kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro Kamishna wa Mamlaka ya Uhifadhi ya Ngorongoro
(NCAA) Dkt. Elirehema Doriye amsema kukamilika kwa nyumba hizo kunaongeza
chachu ya mamlaka kuendelea kuhamasisha na kuhamisha wananchi.
Mapema Kamanda wa Operesheni wa Ujenzi wa nyumba hizo kanali Sadiki Mihayo alimweleza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt.Hassan Abbasi kwamba ujenzi wa nyumba zote 2500 upo hatua za mwisho kukamilika na sasa wanajiandaa kuhamia katika wilaya kijiji cha Kitwai wilaya ya Simanjiro na kijiji cha Saunyi wilaya ya Kilindi kuendelea na ujenzi wa nyumba zilizobaki kulingana na mpango kazi waliojiwekea.
0 Maoni