WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na ujenzi
wa shule ya sekondari ya wasichana ya mkoa wa Iringa na kuagiza Mhandisi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Emmanuel Sigachuma asimamishwe kazi mara moja.
Pia ameagiza Afisa Elimu ngazi ya Sekondari ambaye pia ni
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Nelson Milanzi apewe onyo kwa kushindwa
kusimamia matumizi ya fedha za ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya
Lugalo iliyoko kata ya Mbigili, wilayani Kilolo.
Pia ameagiza Mkurugenzi Mtendaji Mstaafu, Lain Ephraim
Kamendu aitwe ili ahojiwe pamoja na wenzakekuhusu matumizi mabaya ya fedha
hizo. Yeye alistaafu Aprili, mwaka huu na ujanzi ulianza yangu Agosti, 2023.
Amefikia uamuzi huo leo (Jumatatu, Julai 8, 2024) baada ya
kukagua ujenzi wa sekondari hiyo na kukuta kasoro nyingi kwenye madawati,
vyumba vya maabara na bwalo la wanafunzi ilhali walishapewa sh. bilioni tatu za
kukamilisha majengo yote ya shule hiyo.
Kasoro kubwa zilizobainika ni ukosefu wa nyavu za kuzuia mbu
kwenye baadhi ya madirisha wakati mkandarasi ameshalipwa fedha yote, viti na
meza za wanafunzi kupasuka wakati havijaanza kutumika. Viti hivyo vilikabidhiwa
tangu Desemba, 2023 na muda wa matazamio ulikuwa ni miezi sita lakini
mkandarasi keshalipwa fedha zote.
Katika ukaguzi wa bwalo, Waziri Mkuu alielezwa na Mhandisi
Sagachuma kwamba bwalo hilo lilitengewa sh. milioni 774 na wamekwishatumia sh.
milioni 341 hadi kufikia hatua ya linta ambayo alidai ni sawa na asilimia 40 ya
ujenzi wake.
Alipoulizwa fedha zilizobakia ziko wapi, Mhandisi huyo
alijibu kwamba hazipo. Afisa Elimu Sekondari naye hakuweza kueleza ziko wapi au
kama kuna vifaa vilivyokwishanunuliwa vimewekwa wapi.
"Unasema utajenga kwa chuma hapa juu, hizo nondo ziko
wapi? Mabati yako wapi? Majiko yako wapi? Hapa tunatarajia kuwa na watoto 172,
je watakula wapi hawa na masomo yameshaanza?" alihoji Waziri Mkuu bila
kupatiwa majibu.
“Wewe ni Afisa Elimu na kazi yako ni kusimamia ujenzi wa
shule zote, ni kwa nini hukutoa taarifa ya kusuasua kwa ujenzi kwenye Kamati ya
Ulinzi ya Wilaya yako? Taarifa nilizonazo ni kwamba Mkurugenzi aliyekuwepo
alikuwa anakupangia kazi kwenye vituo vya mbali ili usije hapa, lakini bado
ulikuwa na wajibu wa kutoa taarifa juu ya mwenendo huo.”
Kwenye ujenzi wa maabara za shule hiyo, Waziri Mkuu amehoji
ni kwa nini mifereji ya kupitisha gesi na maji machafu imezibwa yote. “Mifereji
haina vishikio, wamejaza matofali hata mwalimu akitaka kukagua mifumo ya gesi
au mifereji ya maji machafu hawezi kuinua hilo tofali. Mifuniko ya mifereji
inayopitisha maji, bomba za umeme na gesi kwenye maabara ya shule hiyo itolewe
na irekebishwe upya,” ameagiza.
Amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Joachim Nyingo asimamie
zoezi la kurudisha madawati yaliyoletwa ambayo ni mabovu kwa gharama za
mkandarasi ili yaletwe mengine mapya. Madawati (meza na viti vyake) mengi
yalikuwa yamepasuka katikati au pembeni na yalikuwa yamepangwa darasani.
“Nimeagiza fundi aliyejenga madirisha atafutwe, aletwe ili aweke nyavu kwenye jengo la utawala. Aliyetengeneza madawati aitwe akayatengeneze upya madawati hayo kwa viwango vinavyotakiwa na kwa gharama zake.”
Pia amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU, Mkoa wa Iringa, awahoji
watumishi hao na aanze uchunguzi mara moja.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekabidhi hati ya
kiwanja chenye ukubwa wa ekari 50 kwa uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara
(CBE) ili waweze kuanza ujenzi wa tawi la chuo hicho katika wilaya ya Kilolo,
mkoani Iringa.
0 Maoni