Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi,Uenezi na
Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, amesema kuwa Chama hicho kipo tayari
kumpokea Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Nassor Ahmed Mazrui
endapo atafukuzwa uanachama katika chama chake.
Kauli hiyo ameitoa leo baada ya kuwepo kwa tetesi za
maandalizi ya kufukuzwa kwa kiongozi huyo kwa madai ya kutoridhishwa na kauli
yake aliyotoa hivi karibuni ya kumpongeza Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi
kwa kazi kubwa ya kuimarisha sekta ya Afya Zanzibar wakati wa uzinduzi wa
nyumba za Wafanyakazi wa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoa wa Kusini Pemba.
Katibu huyo alisema amepokea taarifa kutoka katika chanzo
cha kuaminika kutoka ndani ya ACT-Wazalendo, kuwa jana baadhi ya viongozi wa
Kamati Kuu ya Chama hicho wamekaa kikao cha siri kujadili kwa kina tuhuma
zinazomkabili Naibu Katibu Mkuu huyo Nassor Mzrui na idadi kubwa ya wajumbe hao
walipendekeza afukuzwe kwani kauli zake zinaipigia kampeni CCM na kuwatosa
baharini ACT-Wazalendo.
Mbeto, alisema Chama Cha Mapinduzi ni mwalimu na kinara wa
demokrasia nchini hivyo kipo tayari muda wowote kuwapokea viongozi mbalimbali
wa vyama vya upinzani wanaokiri kwa vitendo na kuunga mkono kazi nuzi ya
kuwaletea maendeleo wananchi bila ubaguzi wa kisiasa.
Katika maelezo yake Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi Mbeto,
alisema kitendo cha kiongozi huyo Nassor Mazrui kutamka hadharani kuwa kura ni
siri hivyo wananchi wana uhuru wa kuchagua chama kinacholeta maendeleo mbele ya
Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi imekuwa ni pigo na majanga kwa ACT-Wazalendo
kutokana na sera zao za kubeza, kupotosha na kukosoa na kutengeneza propaganda chafu ndidi ya CCM
na Serikali zake.
"CCM ni kimbilio la wanasiasa na wananchi wote jambo la
msingi ni kuheshimu na kufuata itikadi na sera zetu kwa kutanguliza mbele dhana
ya ukweli na uzalendo uliotukuka.
Niwambie wananchi kuwa muda wowote tupo tayari kumpokea kwa
mikono miwili Waziri wa Afya na Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Nassor
Mazrui, atakapofukuzwa rasmi na Chama chake kwani sababu ya kufukuzwa kwetu
tunamuona ni shujaa wa kisiasa na mwenye misimamo isiyoyumba,” alisema Mbeto.
Alieleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984
kila mwananchi yupo huru kutoa maoni hivyo hata ndani ya vyama vya siasa kila
kiongozi ana haki ya kutoa maoni yake binafsi na bila kuathiri misimamo ya
Chama chake.
Alitoa wito kwa viongozi wengine ndani ya ACT-Wazalendo
waendelee kujitokeza hadharani kuunga mkono msimamo wa Nassor Mazrui, kwani
hiyo ndio njia pekee ya kujitoa katika jela na utumwa wa kidemokrasia ndani ya
chama hicho.
Alisema wakati umefika wa vyama vya upinzani nchini kuachana
na siasa za ulaghai na propaganda chafu za upotoshaji badala yake wabadilike na
kujenga utamaduni wa kukosoa kwa heshima na kutoa maoni ya kutatua changamoto
za wananchi.
Pamoja na hayo Mbeto, alifafanua mapinduzi ya kisiasa ndani ya vyama vya upinzani yataletwa na viongozi wachache wenye dhamira na misimamo imara na kujitolea katika kulinda maslahi ya wananchi wengi badala ya kundi la viongozi wachache wanaofanya uwakala na udalali wa kisiasa kwa maslahi ya baadhi ya nchi za kigeni.
Sambamba na hayo alisema CCM itaendelea kuheshimu misingi ya kidemokrasia pamoja na kusimania kwa vitendo sera zake ziendelee kuwa na manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Na. Mwandishi Wetu- Zanzibar
0 Maoni