Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua vitabu vya historia ya
Bunge ambavyo vitasaidia kuhamasisha tafiti na kujua zaidi kuhusu mchango wa
Bunge katika maendeleo ya jamii nchini.
Amesema kuwa vitabu hivyo pia vitakuwa kielelezo cha
mafanikio na changamoto ilizopitia Bunge la Tanzania katika kudumisha
demokrasia na utawala wa sheria. “Historia yetu ni sehemu ya mchango wetu kwa
jumuiya ya kimataifa katika kukuza amani, utulivu na maendeleo.”
Amesema hayo leo (Jumatano, Juni 26, 2024) wakati wa
uzinduzi wa vitabu viwili vya historia ya bunge katika ukumbi wa Pius Msekwa,
Jijini Dodoma.Vitabu vilivyozinduliwa ni Kitabu cha Historia ya Bunge kutoka
1926-2024 na Wabunge wa Tanzania na nafasi zao kuanzia mwaka 1965-2023
“Kumbukumbu za historia ya Bunge zinaweza kuchochea utafiti
wa kitaaluma na maendeleo ya nadharia za kisiasa na utawala. Watafiti wanaweza
kutumia taarifa hizi kujenga ufahamu mpya na kupendekeza mifumo bora ya
kisiasa.”
Kwa upande wake Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amepongeza
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa sehemu ya maono ya bunge ikiwemo
kuridhia kulikabidhi bunge maeneo yote yanayozunguka jengo la bunge.
“Tunatarajia kujenga makumbusho ya bunge ambayo yatakuwa ni makubwa kwa nchi nzima ili mtu anapokuja bungeni apate historia ambayo tumeipitia kama nchi lakini pia historia ya bunge letu.”
0 Maoni