Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Tumaini Haonga amesema moja ya maeneo muhimu ambayo Serikali imejipambanua katika Sekta ya Afya ni eneo la lishe kwa vijana balehe.
Dkt. Haonga amebainisha hayo jana wakati akizungumza katika Kikao baada ya kutembelewa na Wadau kutoka Nutrition International kwenye ukumbi wa Ofisi ya Idara ya Kinga uliopo Itega Jijini Dodoma kilicholenga kujadili afua mbalimbali za lishe kwa vijana balehe.
"Moja ya afua muhimu katika sekta ya afya ni afua ya
lishe hususan kwa vijana balehe ,hivyo kwenye eneo hili ni eneo muhimu sana,
maana mtu hususan kijana balehe anapokuwa na lishe bora anakuwa na uwezo wa
kufanya na kuchanganua mambo mfano kufanya vizuri darasani kwa umuhimu huo
zinahitajika nguvu za pamoja katika
kuwekeza suala la lishe,"amefafanua Dkt. Haonga.
Aidha, Dkt. Haonga amesema Serikali itaendelea kushirikiana
na wadau kwani wana mchango mkubwa katika utekelezaji wa afua mbalimbali
ikiwemo afua za lishe.
"Katika utekelezaji wa afua mbalimbali za afya Serikali
imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Nutrition Internation hivyo
ninyi ni moja ya wadau muhimu na tutaendelea kushirikiana nanyi na katika eneo
hili la lishe ni moja ya kipaumbele muhimu," amesema Dkt. Haonga.
Tumekuwa na mkutano wenye mafanikio makubwa kati ya Wizara
ya Afya na wawakilishi kutoka shirika la Nutrition International leo tarehe 24
Juni 2024. Lengo la mkutano huu lilikuwa kuendeleza majadiliano ya afua za
lishe kwa vijana balehe ili kuboresha hali ya lishe kwa vijana balehe nchini.
Wizara ya Afya pia iliwakilishwa na mkurugenzi msaidizi wa huduma za lishe na
wawakilishi kutoka Idara ya Huduma za Mama na Mtoto.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Lishe kwa
Vijana balehe kutoka Shirika la Nutrition International (NI), Dkt. Anjali
Bhardwaj amesema wataendelea kufanya
kazi kwa karibu na Wizara kutekeleza afua za lishe kwa vijana balehe.
NI inaelekeza Mipango ya serikali ili kuhakikisha muendelezo
hata baada ya miradi kufikia ukomo.
Mkurugenzi wa Nutritional International Dkt. George Mwita, ameahidi kuendeleza ushirikiano huo.
0 Maoni