Saadani yaanza kutumia teknolojia kuwadhibiti tembo wasitoke hifadhini

  

Hifadhi ya Taifa ya Saadani imeanza mpango wa kudhibiti wanyamapori, wakiwemo Tembo wasivamie maeneo ya makazi ya wananchi kwa kuwavalisha mikanda ya kielektroniki yenye kutoa ishara ya utambuzi walipo hasa kama wameondoka katika hifadhi.

Taarifa ya kutekelezwa kwa mpango huo imetolewa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, John Nyamuhanga ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Mashariki wakati wa utekelezaji wa zoezi la kuwafunga Mikanda ya Mawasiliano makundi mbalimbali ya wanyama waharibifu.

Kamishna Nyamuhanga amesema, zoezi hilo ni mikakati ya makusudi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori TAWIRI katika kupunguza migongano baina ya wanyamapori na wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi za Taifa.

Alisema, “Matumizi ya teknolojia za kisayansi za kuwavalisha Wanyamapori wakali na waharibifu mikanda yenye mfumo wa mawasiliano itatusaidia kutambua na kudhibiti mienendo yao kabla  ya kusababisha madhara kwa jamii.”

Awali akizungumzia teknolojia hiyo, Mtafiti kutoka TAWIRI, Dk Justin Shamanche amesema kifaa hicho kinauwezo wa kutoa ishara pindi mnyama anapokaribia maeneo ya makaz ya watu hivyo kutoa fursa kwa askar na maafsa wa uhifadhi kwenda kuwadhibiti nakuwarudisha katika maeneo ya hifadhi.

Naye, Afisa Uhifadhi Mwandamizi kutoka Hifadhi ya Taifa Saadani, Prisca Elisia amesema pamoja na kusaidia wanyama hao wasilete vurugu katika maeneo jirani na hifadhi pia inasaidia sekta ya utalii kwa kutambulisha wanyama wapo wapi hivyo kuwa rahisi kwa watalii kufika walipo na kuwaona.

"Teknologia hiyo itasaidia sekta ya utalii kwa wageni kuweza kumuona mnyama wanaemtaka kwa wakati badala ya kumtafuta mnyama kiholela," alisema Prisca.

Naye, Mwakilishi kutoka Kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo, Jeremia Mponji alifurahishwa  kwa teknolojia hiyo kwani wamekuwa wakipata hasara sana katika mashamba yao ya miwa pindi tembo hao walipokuwa wakitoka nje ya Hifadhi .

Alisema kuwa mashamba yao yamekuwa yakivamiwa sana na Tembo  hivyo kuja kwa teknolojia hiyo anaamini itawasaidia maafisa na askari wa uhifadhi kuwaswaga  na kuwarudisha hifadhin Tembo hao  kwa urahisi zaid tofauti na awali .

Hifadhi ya Taifa Saadani ni miongoni mwa Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba nchini ambayo wanyamapori wake wameshafungwa mikanda ya mawasilino ili kuthibiti wanyama hao wasilete madhara kwa wananchi. 

Na. Zainab Ally - Saadani

Chapisha Maoni

0 Maoni