Rais wa Shirikisho la wafugaji Nyuki Duniani (Apimondia),
Dkt. Jeff Petiz, ametembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kutoa pongezi kwa
uongozi wa NCAA kwa jitihada za utunzaji wa hifadhi hiyo ya kipekee duniani
ambayo imeendelea kuvutia maelfu ya watalii.
Akizungumza kwa furaha na mshangao, Dkt. Petiz
amebainisha kuwa hajawahi kuona sehemu
nzuri kama Kreta ya Ngorongoro maishani mwake baada wa kuona wanyama wakubwa maarufu kama Big Five ambao ni faru, tembo, Simba, Chui,
Nyati na wengineo ndani ya mda mfupi wakiwa katika eneo moja wakiwa kwenye
mazingira yao ya asili.
"Hakika nimepata uzoefu usiosahaulika maishani mwangu,
kuona eneo la pekee lililotunzwa na kuwepo wanyama wa kila aina na kushuhudia
idadi kubwa ya wageni ni jambo la kupendeza na hakika eneo hilo kila mmoja
anapaswa kulitembelea katika uhai wa maisha yake," alisema Dkt. Petiz.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Misitu
Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo aliyembatana na mgeni huyo ameipongeza
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhifadhi
eneo hilo mashuhuri duniani katika nyanja za utalii, uhifadhi na utamaduni
pamoja na kupambana na mimea vamizi na kutoa rai kwa taasisi nyingine za
uhifadhi kujifunza kutoka kwa Ngorongoro ili kubadilishana uzoefu.
Ziara hiyo imefanyika katika Kreta ya Ngorongoro ikiwa ni
sehemu ya maandalizi ya mkutano wa kimataifa wa wadau wa nyuki (Apimondia)
utakaofanyika mwaka 2027, ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano huo
mkubwa unaotarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 6,000 kutoka mataifa mbalimbali.
Katika ziara hiyo Dkt. Petiz ameambatana na Rais wa Kamisheni hiyo kanda ya Afrika , Bw. David Mukomana.
0 Maoni