Mpina hapoi, aibuka na safari ya kwenda Mahakamani

 

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina anayetumikia adhabu ya kutohudhuria vikao 15 vya Bunge kutokana na kudharau kiti cha Spika na Bunge, ameibuka baada ya kupewa adhabu hiyo na kusema atachukua hatua za kisheria Mahakamani.

Mpina amesema atapeleka malalamiko yake ya kutolewa kwa uonevu bungeni na kutotendewa haki na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa vyombo vya sheria ili vikapime na kutenda haki kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi.

Pia, Mpina amesema atampeleka Mahakamani Waziri wa Kilimo Hussein Bashe na Bodi ya Sukari chini ya Ibara 26 na 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kitendo cha kutoa idhini ya kutoa vibali vya kuagiza sukari kinyume cha sheria na kulisababishia taifa hasara kubwa.

Mpina ambaye ameibuka baada ya kutafakari kwa zaidi ya saa 120 tangu kupewa adhabu hiyo, amesema pia atayafikisha Mahakamani makapuni yote yaliyojihusisha kuingiza sukari nchini kinyume cha sheria.


Chapisha Maoni

0 Maoni