MAANDALIZI ya michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na
Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) yameanza ambapo Kamati ya Utendaji
imependekeza michuano hiyo kufanyika Septemba 2024 mkoani Morogoro.
Timu zinazoshiriki michezo hiyo zimehimizwa kufanya maandaalizi
kwa watumishi wa serikali kutoka kwenye wizara, taasisi, wakala za serikali,
ofisi za wakuu wa mikoa na halmashauri na manispaa ili kushiriki bonanza la
uzinduzi litakalofanyika Agosti jijini Dodoma na hatimaye michuano ya SHIMIWI
mkoani Morogoro.
Katibu Mkuu wa SHIMIWI, Alex Temba amesema mgeni rasmi wa
bonanza hilo anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka
ambaye ni mlezi wa Shirikisho hilo.
Temba amesema michezo itakayofanyika kwenye bonanza hilo
litakalofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma ni pamoja na kuvuta
kamba kwa wanawake na wanaume, mpira wa miguu, netiboli na mbio za watu wazima
wenye umri wa kuanzia miaka 55.
“Tarehe rasmi ya michezo yetu pamoja na hili bonanza kubwa
itatangazwa baadaye mwezi huu maana ni utaratibu wetu lazima michezo itanguliwe
na bonanza kubwa lenye kushirikisha watumishi wa umma wenye kushiriki kwenye
michezo hii ya SHIMIWI,” amesema Temba.
Hata hivyo, amezitaka timu kuanza kuandaa timu zao kwa ajili
ya kushiriki kwenye bonanza hilo, ambapo amesema rekodi inaonesha ushiriki wa
klabu kwenye michezo hii unaendelea kuongezeka kutoka 47 kwa mwaka 2021 na
kufikia 62 ilikuwa mwaka 2022, na 2023 kulikuwa na klabu 74.
Kikao hicho kimeudhuriwa pia na Mwenyekiti wa SHIMIWI, Bw.
Daniel Mwalusamba ambaye awali alitoa wito kwa timu kuanza maandalizi ya
michezo ya SHIMIWI, ili kuleta ushindani bora kwa kuzingatia maadili ya
utumishi wa umma.
Mwalusamba amesema kwa kuwa mwaka huu michezo itatanguliwa
na uchaguzi wa Serikali za mitaa, ametoa wito kwa watumishi kuelekeza akili zao
pia katika maelekezo ya watendaji wakuu wa serikali kuhusiana na uchaguzi huu.
0 Maoni