Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Madini
iendelee kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi katika kutafuta
teknolojia mbalimbali za uongezaji thamani madini.
Amesema kuwa kufanya hivyo kutawezesha madini yanayopatikana
nchini kutumika katika kuzalisha bidhaa ambazo zinahitajika duniani kote
kutokana na kuongezeka kwa mahitaji na kuendelea kuongezeka kwa idadi ya watu
duniani.
Ametoa agizo jana wakati alipofunga wiki ya madini
iliyoambatana na Kongamano la Wachimbaji Madini, Mkutano Mkuu wa FEMATA pamoja
na Maonesho ya Madini na Vifaa vya Uchimbaji iliyofanyika katika Kituo cha
Mikutano cha Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa rai kwa Wafanyabiashara,
Taasisi za Elimu, Taasisi za Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na
Wizara ya Madini kuendelea kuweka mikakati ya kuwezesha uwekezaji wa ndani wa
teknolojia mbalimbali nchini zitakazowezesha upatikanaji wa malighafi
zinazohitajika na migodi na shughuli nyingine za madini.
“Kwa kuwa teknolojia duniani inazidi kukua kwa kasi wadau wa
madini waongeze na kuimarisha mtandao na wachimbaji wa kikanda na kimataifa. “Kwakujifungia ndani
peke yetu hatutapata suluhisho lachangamoto tulizonazo bali tutachelewesha
maendeleo yetu.”
Amesema kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto, kero na
adha zinazowakabili wawekezaji na wachimbaji wa madini pamoja na kuhakikisha
wanapata masoko ya uhakika ya kuuza madini pamoja na kuendelea kuwawezesha
wawekezaji wadogo katika Sekta ya Madini kwa kuwaunganisha na Taasisi za Fedha
nchini ili waweze kupewa mikopo.
“Katika hili nitoe
wito kwa taasisi za Fedha nchini kukaa na FEMATA, wapeni miongozo na elimu ya
mitaji ili waweze kuitumia katika kuzipa thamani kazi zao ili ziwe na tija.”
Kwa Upande wake, Waziri wa Madini Anthony Mavunde
amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa nguvu sekta ya
madini ili iendelee kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Amesema kuwa Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Madini
kutoka shilingi bilioni 89 hadi kufikia shilingi bilioni 231. “Mipango yetu
ni kuendelea kufanya tafiti za kina ili
kubaini sehemu yalipo madini, pia tumepanga kununua helkopta ya kisasa ya
itakayobaini kilichopo hadi urefu wa kilomita moja chini ya ardhi pamoja na kujenga maabara kubwa ya kisasa katika sekta
ya madini.”
Pia, Mheshimiwa Mavunde amesema Wizara inaendelea kutekeleza
mpango wa kufuta leseni na maombi kwa wawekezaji waliochukua maeneo makubwa ya
uchimbaji madini lakini hawayaendelezi na kuwapatia Watanzania wenye nia ya
kuchimba ili wanufaike na rasilimali hiyo muhimu.
Naye, Rais wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA)
John Wambura amesema kuwa Tanzania inafursa ya kuwa na Soko la madini Afika kwa
kuwa ina kila sifa ya kufikia hapo na hii ni kutokana na juhudi zilizofanywa na
Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, amesema kuwa katika mwaka 2024-2025 FEMATA imepanga kuendelea kuwaomgezea ujuzi na maarifa wachimbaji wadogo wengi zaidi pamoja na kuwaunganisha na Serikali ili kusaidia kuongeza vipato vyao na Taifa kwa ujumla “Pia tumeandaa vitambulisho ili tuweze kutambua kila mchimbaji alipo na anafanya nini.”
0 Maoni