Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imekamilisha maandalizi
muhimu kwa ajili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ikiwa ni
pamoja na ununuzi wa vifaa vya uandikishaji vinavyojumuisha BVR Kits 6,000.
Hayo yamebainishwa jana tarehe 10 Juni, 2024 jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw.
Kailima, R. K wakati akiwasilisha mada kwenye mkutano wa Tume na Viongozi wa
Dini.
Mkutano huo umefanyika sambamba na mkutano wa Tume na
Taasisi na Asasi za kiraia ikiwa ni muendelezo wa utaratibu wa Tume wa
kuwashirikisha wadau wa uchaguzi kabla ya kuanza rasmi kwa uboreshaji wa
Daftari.
Bw. Kailima amesema BVR Kits hizo zitatumia vishkwambi
kuchukua taarifa za wapiga kura ikiwemo picha, saini na alama za vidole.
“BVR Kits za sasa zinatumia mfumo endeshi wa android na
uzito wake ni kilogramu 18, awali zilikuwa zinatumia mfumo endeshi wa window na
uzito wa kilogramu 35”, amesema Bw. Kailima.
Amesema Mfumo wa Uandikishaji wa Wapiga Kura (Voters
Registration System-VRS) umefanyiwa usanifu na kuboreshwa ili kukidhi aina ya
BVR Kits za sasa ambazo zinatumia programu endeshi ya android.
Wakati akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele amesema, BRV Kits hizo zitakuwa
rahisi kubeba na kufanya zoezi la uboreshaji wa Daftari kuwa rahisi haswa
kwenye maeneo ya vijijini ambapo watendaji hulazimika kubeba vifaa kwa umbali
mrefu.
Amesema mfumo wa teknolojia hii ya BVR hutumika katika
kumtambua mtu na kumtofautisha na mwingine.
Uandikishaji huu wa wapiga kura utahusisha uchukuaji wa alama za vidole
vya mikono, picha na saini na kuhifadhiwa kwenye kanzidata ya wapiga kura.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utazinduliwa mkoani Kigoma tarehe 01 Julai, 2024 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB).
Na. Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
0 Maoni