Jitihada za pamoja katika kukabiliana na ujangili, biashara
haramu ya usafirishaji wa wanyamapori hai na mazao yake; pamoja na mazao ya
misitu ni chachu ya mafanikio katika utekelezaji wa Makubaliano ya Lusaka.
Aidha, nchi wanachama zina wajibu wa kugharamia jitihada hizo bila kuchoka ili
kulinda mafanikio yaliyopatikana.
Haya yamebainishwa na Rais wa Baraza la Uongozi la Mawaziri
wa nchi wanachama wa Makubaliano ya Lusaka anayemaliza muda wake Mhe. Dkt.
Alfred Mutua - Waziri wa Utalii na Wanyamapori wa Jamhuri ya Kenya alipokuwa
akifungua Mkutano wa 13 wa Baraza hilo la Uongozi.
Vilevile katika hotuba yake Mhe. Mutua alitoa pongezi kwa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kujitolea kuteua
na kumgharamia afisa kutoka Tanzania kuwa sehemu ya kikosi kazi kinachoratibu
utekelezaji wa shughuli za kila siku za Makubaliano ya Lusaka yanayolenga kuwa
na mikakati ya pamoja katika kupambana na wimbi la biashara haramu ya
wanyamapori hai, nyara na mazao ya misitu.
Aidha, akiushukuru uongozi wa Baraza la Uongozi la Mawaziri
kutoka nchi wanachama wa Makubaliano ya Lusaka, Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) ambaye alimuwakilisha Mhe. Angella J. Kairuki
(Mb) - Waziri wa Maliasili na Utalii alisema kuwa kikosi kazi kinachoratibu
utekelezaji wa shughuli za kila siku za Makubaliano ya Mkataba wa Lusaka
kimefanya kazi kubwa katika kuimarisha shughuli za uhifadhi kwa kubuni mbinu
mpya za kupambana na ujangili wa wanyama pori na mazao ya misitu.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya
nchi wanachama katika kupashana habari na jitihada za pamoja kupambana na
ujangili na mienendo ya biashara haramu kumewezesha kudhibiti na kupunguza
vitendo vya ujangili na biashara haramu; na hivyo kulinda na kuhifadhi maliasili
za bara la Afrika.
Mhe. Kitandula alitumia nafasi hiyo kuzikakaribisha nchi
wanachama wa Makubaliano ya Lusaka kushiriki kwenye mkutano wa 14 unaotarajiwa
kufanyika nchini Tanzania mwaka 2025.
“Nashauri kikosi kazi kiendelee kutoa elimu kwa nchi nyingi
zaidi ili zijiunge kwenye kutekeleza makubaliano ya Lusaka na hivyo
kulinda na kuhifadhi maliasili zilizopo katika bara la Afrika kwa vizazi vya
sasa na vizazi vijavyo,”alisema Kitandula.
Mkataba wa Makubaliano ya Lusaka ambao utekelezaji wake ulianza miaka 13 iliyopita una lengo la kupambana na kuzuia biashara haramu ya usafirishaji wanyamapori hai na mazao yake pamoja na usafirishaji haramu wa mazao ya misitu.
Na. Anangisye Mwateba-Nairobi Kenya
0 Maoni