Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali imeandaa mpango wa mageuzi ya sekta ya mifugo ambao utasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo nchini.
Ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kubuni mbinu na mikakati
ya kuondokana na ufugaji usio na tija na kuwezesha kufuga kisasa.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Juni 16, 2024 Kibaha, Pwani
wakati akifunga Maonesho na Mnada wa Mifugo kwa mwaka 2024.
“Wizara msichoke wala msiache kuwapa elimu wafugaji wetu,
lazima tukubali kuwa wamekuwa hivyo kwa
miaka mingi mabadiliko lazima yatokee na lazima tujue kuwa maeneo mengi yanayohitaji ardhi
yanaongezeka ikiwa ni pamoja na mifugo lakini ardhi haiongezeki. Hivyo,
tuendelee kuwapa elimu ya ufugaji wa kisasa
na kuwahimiza wafugaji waje kwenye maonesho kama haya ili wapate
ujuzi na teknolojia itakayowasaidia,” amesema
Dkt. Biteko.
Amesisitiza “ Wafugaji tujue kwamba nchi na dunia
inabadilika ni vizuri tukabadilika sasa kabla mabadiliko yenyewe
hayatulazimisha kubadilika kama tumeamua ufugaji ni maisha yetu lazima tuamini
maisha yamebadilika tuwe na mifugo yenye tija ambayo itatuletea fedha
zitakazoweza kubadilisha maisha yetu.”
Ameendelea kusema “Wafugaji msijione dhaifu wala wanyonge
unaweza kukuta mfugaji ana ng’ombe 1,000 huyo huwezi kumuita masikini, ng’ombe
hao wanaweza kuwa mtaji kinachohitajika ni namna gani unaweza kubadilisha
maisha yako kwa kutumia hao ng’ombe ulionao.”
Vilevile, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea
kufanya jitihada mbalimbali ili kuboresha sekta ya mifugo nchini ikiwa ni
pamoja na kutenga maeneo maalum kwa ajili ya malisho ya mifugo huku akiwaasa
wafugaji kuepuka kuwa na migogoro baina yao na wakulima kwa kuwa wanategemeana
na migogoro hiyo inaathari kijamii na kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa ni vyema
maonesho hayo ya mifugo yakafanyika kikanda ili yaweze kuwafikia wakulima wengi
zaidi nchini ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili
mfano mbegu bora za mifugo au kujua teknolojia za kisasa za ufugaji.
Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti
amewapongeza washiriki na wadhamini wa maonesho hayo ya mifugo ambayo yanalenga
kutoa elimu kwa wafugaji ili kuleta tija.
“Maonesho haya ni ya muhimu na kwa mwaka huu tumeyawekea
nguvu zaidi kwa kuwa yanaleta matokeo
makubwa na kwa kuwa yamekuwa maelekezo ya viongozi wetu wa Serikali kuwa
wafugaji wetu wasifuge kizamani. Lazima sasa ifike mahali wafugaji wetu waondokane
na ufugaji wa kizamani kwa mwamvuli wa kimila, na sisi Wizara tumekuwa tukitoa
elimu mara nyingi kupitia wataalamu wetu
na Maafisa Ugani licha ya wafugaji hawa kuwa na mwamko mdogo wa kufuga
kisasa,” amesema Mhe. Mnyeti.
Ametolea mfano kuwa wafugaji hutembea umbali mrefu kutafuta
malisho na matokeo yake mifugo inafika ikiwa imechoka na kuwa Serikali
imeendelea kutenga maeneo ya malisho ili kusaidia wafugaji nchini.
“Tunatoa elimu ya kufuga kisasa kwa kunenepesha mifugo na
kuuza hata ng’ombe mmoja kwa shilingi 500,000 au zaidi badala ya shilingi
200,000. Wafugaji lazima wajue ng’ombe ambaye hajafugwa kisasa, hajapata chanjo
au akiugua anapewa tu dawa kiholela hawezi kuuzwa nje ya nchi kwa sababu hana
ubora,” amesema Mhe. Mnyeti.
Pia, amewataka wafugaji nchini kuwatumia wataalamu wa mifugo
ili waweze kupewa elimu ya ufugaji wa kisasa na wenye tija ili kubadilisha
sekta ya mifugo nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ambaye pia ni Mbunge
wa Jimbo la Chalinze, amesema kuwa ni
wakati sasa wafugaji wanatakiwa
kubadilika kwa kufanya ufugaji wa kisasa kwa kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea
kuhakikisha sekta ya ufugaji inapata mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na
kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafugaji Kibiashara Tanzania, Bw.
Naweed Mulla amesema kuwa Jumuiya hiyo inalenga kuwakutanisha pamoja wafugaji,
kupeana ushauri na kusaidiana kwenye
changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuisaidia Serikali iweze kuwafikia
kirahisi wakati wanapohitaji msaada.
“Jumuiya hii inatusaidia sana na ningependa kuishukuru Serikali
inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na watendaji wote wa Wizara
hii ya Mifugo na Uvuvi kwa kutusaidia wafugaji ili sasa tuweze kufuga
kibiashara,” amesema Bw. Mulla.
Ameeleza kuwa mtu anapotaka kufanya mambo makubwa lazima
watu wengine watakosoa hivyo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aendelee
kufanyakazi kwa kuwa Jumuiya ya Wafugaji Kibiashara Tanzania itaendelea
kushirikiana na Serikali ikiwa ni pamoja na kuleta mabadiliko katika sekta ya
mifugo na kuwa ufugaji wa kizamani hauna tija.
Awali, Dkt. Biteko ametembelea mabanda mbalimbali ya
maonesho ikiwemo banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Rachi ya Mbogo
sambamba na kushuhudia mnada wa ng’ombe.
Maonesho na Mnada wa Mifugo kwa mwaka 2024 yaliyofanyika kwa siku tatu yalizinduliwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti.
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni