Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi
amewaongoza watumishi wa wizara hiyo kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu
anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula aliyeteuliwa hivi karibuni baada ya
kuwasili kwenye Ofisi yake mtumba Mtumba jijini Dodoma.
Mara baada ya kuwasili alipokewa na watumishi wote wa Wizara
hiyo na baadaye kufanya kikao na menejimenti ya Wizara.
Akimkaribisha ili aweze kuzungumza na Menejimenti Dkt.
Abbasi, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu
Hassan kwa maono yake ya kuboresha sekta ya utalii ambayo imekuwa na mchango
kwenye uchumi.
Amemshukuru kwa kumteua Mabula ili aweze kusaidia sekta ya
utalii ili kuimarisha na kuboresha sekta hiyo ambayo yeye mwenyewe amekuwa
akiipambania.
"Kipekee napenda kumshukuru Mhe. Rais kwa kutuongezea
nguvu katika eneo hili, sisi tunamshukuru na kumpongeza kwa maono yake makubwa
kwenye sekta ya utalii kwani yeye mwenyewe amekuwa mwongoza Utalii namba moja.
Akitoka ofisini akapanda milima na mabonde, akacheza filamu ya The Royal Tour,"
amefafanua Dkt. Abbasi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Abbasi amemkabidhi vitendea kazi
ikiwa ni pamoja na miongozo mbalimbali kama sera na kanuni za sekta ya utalii.
Kwa upande wake, Mabula amewashukuru watumishi wote na kuomba ushirikiano ili kufanya kazi kwa weledi.
Na John Mapepele- Dodoma
0 Maoni