Ruto alaani ghasia, Uhuru ashauri wananchi wasikilizwe

 

Rais wa Kenya William Ruto amelaani ghasia zilizotokea jana wakati wa maandamano ya vijana ya kupinga muswada wa fedha wa nchi hiyo, uliopitishwa na bunge la nchi hiyo.

Vijana hao waliojipanga kwa maandamano yaliyoratibiwa kupitia makundi ya WhatsApp walivamia bunge, kuvunja vitu kung’oa bendera pamoja na kuondoka na siwa na vazi la spika wa bunge.

Katika hotuba yake aliyoitoa Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto amesema tukio hilo ni shambulizi la demokrasia ya Kenya, utawala wa sheria pamoja na uadilifu wa taasisi za kikatiba.

“Shambulizi la leo la mamlaka ya kikatiba limesababisha kupotea kwa uhai wa watu, uharibifu wa mali, na kutoheshimu mihimili pamoja na nembo ya taifa,” alisema Ruto.

Rais Ruto aewaonya wahusika wa ghasia kuwa serikali itachukua hatua kali dhidi yao, na kuvipongeza vyombo vya dola kwa jitihada zao za kuilinda nchi.

Kwa upande wake Rais Mstaafu wa Kenya wa awamu ya nne Uhuru Kenyatta amewasihi viongozi kuwasikiliza wananchi ambao ndio waliowaweka madarakani.

“Viongozi wanapaswa kujua kwamba wamechaguliwa na wananchi, hivyo kuwasikiliza wananchi si suala la kujiamulia bali ni lazima, kikatiba na kidemokrasia,” amesema Uhuru.

Amewataka viongozi wote kuonyesha ustahamilivu, na kufanya jambo sahihi la kuwasikiliza watu badala ya kujenga uhasama, kwani ghasia sio jibu.

WANAWAKE WAANDAMANA

Kwa kawaida wakati wa maandamano kama hayo nyakati za nyuma waandamanaji walikuwa ni wanaume na wanawake walikuwa wanajificha majumbani kunusuru maisha yao.

Hata hivyo safari hii wanawake walikuwa bega kwa bega na wanaume na kuvunja mwiko wa maandamano kuwa ni ya wanaume pekee.

Vijana wa kike na wa kiume wameshiriki kikamilifu maandamano hayo ya vuguvugu la vijana wa kizazi cha Gen Z, ambayo wamesababisha shughuli nyingi kusimama kwa siku kadhaa nchini Kenya.

Mabinti hao majasiri na imara wamekabiliana kikamilifu na vyombo vya dola na kuhakikisha sauti zao zinasikika katika kupinga muswada huo wa fedha.

Kwa mujibu wa Tume ya Haki za Binadamua Kenya (KNHRC) watu wapatao 22 walifariki katika maandamano yaliyofanyika jana.


Chapisha Maoni

0 Maoni