Waziri Kairuki ampongeza Rais Samia kwa kutoa magari kwa kanda zote za TFS

 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe Angelah Kairuki amempongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa magari 22 kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yatumike kwenye  usimamizi wa raslimali za misitu  nchini  ili kuwakomboa  wanawake waachane na nishati chafu za kuni na mkaa ambazo zimekuwa zikiwaletea changamoto nyingi na kinara wa matumizi  ya nishati safi Afrika.

Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo leo Mei 24 wakati alipokuwa akikabidhi kwa  menejimenti ya TFS magari 22  yaliyonunuliwa wa Serikali yatakayotumika katika usimamizi wa misitu katika kanda zote saba  hapa nchini yenye thamani ya shilingi bilioni 4.3 ikiwa  ni  Toyota Prado VXL,  7 zilizogharimu  shilingi  bilioni 2.2 kwa ajili ya Wakuu wa Kanda hizo na Toyota LandCruiser Hardtop, 12 zilizogharimu  shilingi  bilioni 2.1 zitakazotumika na Maafisa  kwenye  maeneo yote ya kanda. Hiyo ikiwa ni awamu ya kwanza ambapo awamu ya pili serikali itatoa magari tisa aina ya Toyota LandCruiser Hardtop.

Amefafanua kuwa ukiachana na uharibifu  wa mazingira unaotokana  na matumizi ya nishati chafu ya kupikia kama kuni na mkaa  tumeendelea kushuhudia  majanga mengi  yakitokea katika mazingira  na afya  ya binadamu ambapo mwanamke  amekuwa mhanga mkubwa  wa  masuala haya  kwa sababu  kwa kiasi  kikubwa  ndiyo watafutaji na watumiaji wa  nishati chafu za  mkaa na kuni  zinazotokana na ukataji wa misitu hivyo magari hayo yametasaidia kwenye doria na usimamizi wa raslimali za misitu.

Ameongeza kuwa kutokana na umuhimu huo, Mei nane mwaka huu, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi mkakati wa miaka 10 wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia kutoka mwaka 2024 hadi 2034 unaohusisha  pia masuala mbalimbali ikiwemo  kuongeza uelewa wa wananchi kutumia Nishati Safi ambao umelenga  kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 zaidi ya asilimia 80 ya wanawake wote nchini waweze kutumia  nishati safi.

Ametaka  magari hayo yawe chachu ya kuwaongezea ari  ya kufanya kazi kwa ubunifu, bidii na maarifa na  kufika maeneo  ya mbali zaidi huku wakiyatumia kwa uangalifu ili kuleta tija iliyo kusudiwa ya  kutoa elimu ya uhifadhi wa misitu, kufanya doria za kimkakati na kufanya usimamizi wa raslimali za  misitu kwa ujumla.

Aidha, ameitaka TFS kufikiria kuanzisha mazao mapya ya utalii wa ikolojia, miundombinu ya malazi kwa wageni na kuchangamkia biashara  ya Cabon huku wakiendelea kuandika maandiko ya miradi ili kuliingizia fedha taifa.

Amesema ni muhimu kuthamini na kutekeleza kwa vitendo maono ya Mhe. Rais ya kutangaza Tanzania kama alivyofanya kwenye Filamu ya The Royal Tour na hivi Karibuni Filamu ya Amaizing Tanzania iliyozinduliwa Beijing China Mei 15 mwaka huu.

Awali, akimkaribisha Mhe.Waziri Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, CP Benedict Wakulyamba ambaye ndiye Msimamizi Mkuu wa Jeshi la Uhifadhi amemshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kuijengea uwezo TFS kwa kutoa fedha nyingi kununua vitendea kazi vya kisasa vya kufanyia kazi ya uhifadhi.

“Naomba niwe muwazi, katika kipindi chote cha utumishi wangu, katika kipindi hiki kifupi cha Mhe. Rais Samia amefanya maboresho ya kisasa kwa kusaidia kuleta vifaa vya kidigitali na magari, ninamshukuru na kumpongeza sana Mhe. Rais,” ameongeza CP Wakulyamba. 

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dosantos Silayo amemhakikishia Waziri Kairuki kuwa Menejimenti yake imejipanga vizuri ili kuhakikisha kuwa magari hayo yatakwenda kuongeza ufanisi mkubwa na kuliingizia taifa mapato zaidi.

Amesisitiza kuwa kwa sasa TFS inatumia teknolojia ya kisasa ambayo itasaidia kuboresha  usimamizi wa  maeneo makubwa ya misitu na nyuki  hapa nchini.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mwakilishi wa Mwenyekiti  wa Bodi ya TFS,  Dkt. Siima Makengeza, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili Deusdedith Bwoyo, Wasimamizi wa kanda zote saba za TFS na  maafisa mbalimbali wa  Wizara.

Na. John Mapepele


Chapisha Maoni

0 Maoni