Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.
Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa wafanyakazi wa SMZ wataongezewa posho ya
shilingi 50,000 ya nauli ili kuleta ufanisi katika kazi na kurahisisha masuala
ya usafiri kwa ajili ya nauli za kwenda kazini na kurudi nyumbani.
Amesema shilingi bilioni 34 zimetengwa na Serikali kwa ajili
ya posho ya usafiri kwa watumishi wote wanaostahiki kulipwa posho.
Rais Dk. Mwinyi amesema hayo
katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani (Mei Mosi)
zilizofanyika jana kwenye uwanja wa Gombani, Mkoa wa Kusini Pemba tarehe 1 Mei
2024.
Aidha Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali imejipanga
kutengeneza ajira 300,000 kwa wananchi wake
kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Halikadhalika Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa katika kipindi
cha miaka mitatu Serikali kupitia shughuli utekelezaji wa miradi ya maendeleo ajira
mpya zipatazo 187,651 zimepatikana sawa
na asilimia 104 ya lengo la ajira 180,000 kwa miaka mitatu iliyopita.
Kwa upande mwingine Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha inaongeza fedha kwa ajili ya posho ya likizo , zikiwa zimetengwa shilingi bilioni 2.5 katika bajeti mpya ya mwaka 2024/25.
0 Maoni