Katika kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu kama
Mei Mosi, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), jana tarehe 01 Mei,
2024 imetembelea Kituo cha Watoto wenye uhitaji cha CHAKUWAMA kilichopo Sinza
jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa msaada wa vifaa mbalimbali.
Akikabidhi msaada huo
kwaniaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Afisa Habari Mkuu Bi.
Christina Njovu alieleza kuwa Wakala imetoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa sera ya kurudisha kwa
jamii ambapo wakala imekuwa ikiitekeleza mara kwa mara.
Baadhi ya vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na vyakula
vikiwemo unga, sukari,vifaa vya usafi na vifaa vya shule.
Naye Mkuu wa Kituo cha CHAKUWAMA Bw. Hassan Hamis
ameishukuru BRELA kwa kufika kituoni hapo kuwatembelea na kwa msaada uliotolewa
ambao umewapa faraja kubwa ikizingatiwa kwamba hivi karibuni wamepatwa na janga
la moto kwa kuunguliwa na bweni la kulala Watoto.
Aidha, Bw. Hamis ameeleza kuwa, Kwa sasa kituo kina watoto
72 wa jinsia zote wenye umri tofauti kuanzia chini ya mwaka mmoja hadi miaka 19
na wengi wao wanasoma shule ya msingi na sekondari na kwamba changamoto zao ni
nyingi hivyo ujio wa BRELA na vifaa ilivyotoa vitapunguza ukali wa baadhi changamoto zinazowakabili.
Akielezea historia ya kituo hicho Bw. Hamis.amesema kuwa,
Kituo kilianza mwaka 1998 kikiwa na Watoto 5 chini ya mwanzilishi Bi. Saida
Hassan kikitumia nyumba ya kupanga eneo la Mikocheni , Kituo kimesajiliwa na kinafanya kazi kwa
karibu na Wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia Watoto na makundi maalum.
Na kuongeza kuwa kituo kina watoto aliowatenga katika makundi
sita wakiwemo, yatima waliopoteza wazazi
wote wawili, Watoto waliopoteza mzazi
mmoja, wapo waliotolewa kwenye mazingira hatarishi na wale waliofanyiwa ukatili
na walio okolewa kutoka biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu pamoja na
walemavu.
Katika Watoto 72 watoto 60 wanasoma katika ngazi tofauti
kuanzia chekechea, msingi, sekondari, veta na vyuo katika shule za serikali na shule binafsi za
kulipia.
Pia, Bw.Hamis ameeleza kuwa moja ya changamoto
wanazokabiliana nazo ni pamoja na Watoto 12 wamesimamishwa kuendelea na masomo
kutona na kuathilika kiakili kulikotokana na ukatili waliofanyiwa na wengine
kupata magonjwa na hivyo wanaendelea na matibabu.
Mbali ya kutembelea kituo cha Watoto wahitaji, BRELA pia imeshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani iliyobebwa na kaulimbiu Nyongeza ya mishahara ni msingi wa mafao bora na kinga dhidi ya hali ngumu ya maisha.
0 Maoni